Monday 26 March 2018

UVCCM GEITA YAWAKUTANISHA WATU WENYE ULEMAVU WANAWAKE NA VIJANA KUJADILI ASILIMIA 10 ZINAZOTOLEWA NA HALMASHAURI

Wajumbe wa mkutano ambao ulikuwa umelenga kutoa ufafanuzi juu ya asilimi 10 ambazo zinatolewa na halmashauri kwa wanawake,vijana pamoja na walemavu Wilayani Geita.

Katibu wa UWT,Bi Mazoea Salum akielezea akisoma mapendekezo ambayo wameyaadhimia kwenye Kikao hicho.

Katibu wa chama cha mapinduzi(CCM) Wilaya ya Geita,Julius Peter Akizungumza na wajumbe kwenye mkutano huo.

Mkuu wa wilaya ya Geita,Mwl Herman Kapufi ambaye alikuwa ni mgeni rasmi kwenye Kongamano hilo akisisitiza suala la uanzishwaji wa viwanda vidogo kwenye vikundi.

Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Geita,Manjale Magambo akielezea umuhimu wa fedha asilimia 10 ambazo zimekuwa zikitolewa na halmashauri kwa vikundi vya vijana ,wanawake na walemavu.

Kundi la watu wenye ulemavu kwenye halmashauri ya mji wa Geita , wamelalamika    kutonufaika na mkopo wa asilimia 2 kutoka kwenye asilimia 10 ya Mkopo  ambao umekuwa ukitolewa kwa wanawake na vijana kutoka kwenye halmashauri hiyo hali ambayo imekuwa ikisababisha kuendelea  kuwa na maisha magumu pamoja na kuendelea kuunda vikundi vya ujasiriamali.

Hayo yamebainishwa wakati wa Kongamano ambalo limeandaliwa na umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM) , jumuiya ya wanawake(UWT) na walemavu  Wilayani Geita,kwa lengo la kujua namna ambavyo makundi hayo yanaweza kunufaika na asilimia 10 ambazo zinatolewa na halmashauri kupitia idara ya maendeleo.

Bw. Mathayo Peter akizungumza kwa niaba ya wenzake ambao wana ulemavu alisema  tangu kuanza kwa mpango huo ni vikundi viwili tu vimekwisha kopeshwa pamoja na kuwa na vikundi vingi na hata wakiulizia juu ya mikopo hiyo wamekuwa wakikutana na majibu ya kuwakatisha tamaa.

“Hii asilimia mbili ilikuwa ni nzuri tatizo linakuja kwenye idara ya maendeleo ya halmashauri ya mji wa Geita kuwepo kwa baadhi ya watumishi kuwa na kauli mbaya dhidi yetu kwani sijui huwa wanatuona hatuwezi lakini mimi niseme na sisi tunaweza kwanza ukizingatia tunazo familia zinatutegemea kwanini wawe wagumu kutupa hiyo mikopo”Alisema Peter.

Aidha kwa upande wake Katibu wa UWT wilayani humo,Bi Mazoea Salum amekiri Kukosekana kwa uwelewa juu ya utoaji wa mikopo kwa vijana ,wanawake na walemavu pamoja na kuwepo kwa urasimu ametaja kuwa ni kikwazo kwa walengwa wa mikopo hiyo kwenye halmashauri ya mji wa Geita hali inayosababisha vikundi vingi kusambaratika.

 Mwenyekiti wa uvccm wilaya Geita Manjale Magambo amewaomba viongozi kusimamia fedha hizo na kutenda haki katika utoaji wa mikopo hiyo ili iweze kuwanufaisha walengwa na kuweza kufikia azma ya serikali ya kuwa Tanzania ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kwa  upande wake afisa maendeleo ya jamii,Bi Valeria Makonda amesema kuwa kundi la watu wenye ulemavu wanalitambua na kwamba hadi sasa wameshatoa mkopo kwenye vikundi viwili na kwamba wataendelea kutoa kutokana na taratibu zilizopo.

Mkuu wa wilaya ya Geita,Mwl Herman Kapufi alifafanua kuwa kutokana na uelewa wa elimu juu ya fedha ambazo zinatolewa na halmashauri ni vyema wahusika wakawa na elimu ya kutosha ya kutambua ni namna gani wanaweza kuzitumia fedha hizo.

No comments:

Post a Comment