Halmashauri ya mji wa Geita inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya
madarasa elfu moja na sabini na tisa (1,079) huku mahitaji yakiwa
ni elfu moja miatano na saba (1,507) na ambavyo vipo ni mianne ishirini na
nane (428) .
|
Hali hii imewasukuma viongozi wa Chama cha mapinduzi (CCM)
Wilayani Geita,kushirikiana na wananchi kwenye ujenzi wa vyumba vya
madarasa kwenye shule ya msingi Kaseni iliyopo Kata ya Mtakuja
Wilayani humo,lengo likiwa ni kupunguza changamoto ambazo zimeendelea kuwakumba
wanafunzi kusomea nje.
Akizungumza wakati wa shughuli hizo ,Katibu wa siasa na uenezi wa CCM,Bw
Jonathan Masele amesema wameamua kufanya hivyo kutokana na ilani ya chama
kuelekeza kushiriki katika suala la maendeleo na kwamba kufanya hivyo
kutasaidia kuwaepusha watoto kukaa nje ya madarasa.
“Tumeamua kwa sababu ilani yetu ya chama cha mapinduzi
inaelekeza kutekeleza majukumu ya wananchi kwa kuwasaidia kujenga mashule
kufanya kazi za mikono ,hii ilani yetu tunaitekeleza ili kuhakikisha watoto
wanasoma kwenye mazingira mazuri” Alisema Masele.
Mwenyekiti wa CCM wilayani humo,Barnabas Mapande amewataka wananchi
kujitolea kufanya kazi za maendeleo na kuachana na dhana ya maandamano
yasiyokuwa na msingi kwa Taifa ,kwani ni vyema kuendelea kuunga mkono juhudi za
Rais za kuboresha miundombinu ya Elimu.
“Tunahitaji kufanya kazi muda wa maneno umekwisha awamu hii ni ya kazi
wanaosema maandamano wakaandamane lakini hutakiwi kuandamana kama unataka
maandamano kasombe mawe, kuchimba msingi tufanye kazi kwa ajili ya watoto wetu
wanaandamana waende huko lakini cha moto watakiona sisi tufanye kazi za
maendeleo” Alisisitiza Mapande.
Aidha Kaimu afisa elimu halmashauri ya mji wa Geita,Mwl Salome Cheleani
ameelezea kuwa wanaendelea na mikakati ya ujenzi wa madarasa na kuyamalizia
maboma ambayo yalikuwa bado hayajakamilika na kwamba wana imani mwaka huu
watapunguza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya vyumba vya madarasa.
No comments:
Post a Comment