Mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya chama cha mapinduzi(CCM) Mkoani Geita Iddi Kassim Iddi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli
amesema Tanzania ni nchi ya tano kwa ukuaji wa uchumi barani Afrika hivyo
wananchi wanapaswa kuwapuuza wanasiasa wanaohubiri kuporomoka kwa uchumi kwa
matakwa ya kujiimarisha kisiasa.
Hayo aliyabainisha kwenye shughuli
ya uzinduzi rasmi wa barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa kilomita 45 ambayo
imekamilika kwa kujengwa kwa kiwango cha lami.
Katika dhifa hiyo iliyofanyika katika Kijiji cha Runzewe Kata ya Uyovu
Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita, Rais Magufuli Alisema katika kipindi cha miaka
miwili serikali imefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta
mbalimbali kwa usimamizi mzuri katika rasiliamali Madini, kuboresha sekta ya
elimu ambapo wanafunzi wanasoma bure kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari.
Alisema kuwa, bajeti ya mwaka 2015 katika sekta ya afya ilikuwa ni
Bilioni 31 lakini serikali kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha afya za
watanzania ambapo sasa bajeti imefikia shilingi Bilioni 239 na hayo ni matokeo
ya umoja na amani iliyopo nchini.
Rais Magufuli ameendelea kusisitiza suala la amani iliyopo
nchini Tanzania kwamba imejengwa chini ya muasisi Hayati Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, ikasimamiwa vyema na marais wastaafu Mhe Ally Hassan
Mwinyi, Mhe Benjamin Mkapa pamoja na Mhe Jakaya Mrisho Kikwete.
"Mambo yanayofanywa na serikali hayawezi kuyafurahisha mataifa
mengine hivyo mataifa hayo yanawatumia watanzania wenyewe kutengeneza chuki
dhidi ya serikali yao" Alisema Rais Magufuli.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo imekuwa sehemu ya Kuchochea
shughuli za maendeleo ya kijamii katika usafirishaji wa mazao, kurahisisha
usafirishaji wa watu na bidhaa, sambamba na kuongeza pato la Mkoa wa Geita
na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Rais Magufulu amewasihi wananchi Kutovamia hifadhi
za Taifa badala yake kuwa wavumilivu na kuiacha serikali ifanye, kwani
watatumwa wataalamu wa Wizara ya ardhi na maliasili ili kuratibu na kuona namna
ya kuyagawa maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima.
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe Elius John Kuandikwa na Mtendaji
Mkuu wa Tanroads nchini Mhandisi Patrick Mfugale walisema kuwa usanifu wa
barabara hiyo ulifanywa mwaka 2006 na kampuni mbili za kitanzania kwa jumla ya
Shilingi Milioni 207.6 ambapo barabara hiyo imesanifiwa kubeba na kutumika kwa
miaka 20 kwa upana wa mita 9.5
Walisema Ujenzi wa barabara hiyo uliokamilika Octoba mwaka jana
umegharimu jumla ya shilingi Bilioni 45.454, ambapo msimamizi amelipwa shilingi
Bilioni 2.3 huku akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa mkandarasi hadi mwezi
Octoba mwaka huu.
Dhifa ya uzinduzi wa barabara hiyo umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita
Mhandisi Robert Gabriel, Naibu Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na
mawasiliano, Mhe Elius John Kuandikwa, Mbunge wa Jimbo la
Bukombe ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph
Nyamhanga na Mtendaji Mkuu wa Tanroads Mhandisi Patrick Mfugale.
No comments:
Post a Comment