Wananchi wa
Kitongoji cha Mahiga, Kijiji cha Mwakitolyo, Tarafa ya Nindo Wilayani
Shinyanga wametakiwa kufanya subira wakati mgogoro wao wa fidia na mwekezaji
ambaye ni Kampuni ya uchimbaji madini ya Henan Afro Asian Engineering
ukitafutiwa ufumbuzi.
|
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko
ametoa wito huo Machi 12, 2018 kwenye mkutano na wananchi hao uliofanyikia
kwenye Kitongoji cha Mahiga na kuhudhuriwa na watendaji mbalimbali wa Serikali.
Mkutano huo unafuatia agizo la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alilolitoa Machi 11, 2018
kwenye mkutano na wananchi wa Kahama ambapo alielezwa na Mbunge wa Jimbo la
Solwa, Ahmed Salum kuwa wananchi wa Mahiga wana mgogoro wa muda mrefu na
mwekezaji hususan kuhusiana na suala la ulipaji fidia ili kupisha mradi.
Kufuatia maelezo hayo ya Mbunge, Rais
Dkt. Magufuli alimuagiza Naibu Waziri Biteko kuhakikisha anafika kwenye eneo
hilo ili kujionea hali halisi na kuwasikiliza wananchi.
Rais Magufuli alisisitiza kuwa ni
wakati sasa Watanzania waanze kunufaika na rasilimali zao ikiwemo madini.
"Tunataka madini yawanufaishe Watanzania," alisema Rais Magufuli.
Alisema wawekezaji wakifika nchini ni
lazima wahakikishe Watanzania wananufaika kwa namna mbalimbali ikiwemo ajira,
kodi na tozo.
"Jukumu langu nimeamua kusimamia
suala hili; Nawahakikishia Serikali iko imara kwa ajili ya kuwatetea
wanyonge," alisema Rais Dkt. Magufuli.
Aliagiza mwekezaji atakayehitaji
kuchimba kwenye maeneo yenye wachimbaji wadogo ni lazima kwanza akubaliane nao
ikiwemo suala la ulipaji wa fidia na sio kuwafukuza.
"Suala la wachimbaji lizingatiwe
kwa mujibu wa sheria. Tuwalee ndio maana tumeanzisha vituo vya mfano maeneo
mbalimbali ili wajifunze," alisema.
Aidha, kwa mujibu wa Mbunge huyo ni
kwamba mgogoro huo ulianza tangu Julai 2017 baada ya mwekezaji huyo kuanza
shughuli zake za kuandaa mazingira ya kuchimba bila kuwa na makubaliano maalum
na wananchi hao.
Akiwa katika mkutano na wananchi hao,
Biteko alielezwa kero mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kutoridhishwa na kiasi
cha fidia kilicholipwa ili kupisha maeneo yao kwa ajili ya mwekezaji, wengine
kutohitaji kabisa fidia na maombi ya baadhi yao kuruhusiwa kufanya shughuli
mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji na uchimbaji kwenye maeneo husika.
Biteko aliwataka kufanya subira wakati
Serikali inatazama namna bora ya utatuzi wa hoja zao kwa mujibu wa sheria ili
manufaa yapatikane bila kumuonea yoyote.
Alisema Rais Dkt. John Magufuli
anataka kuona Watanzania wanyonge wananufaika na rasilimali zao ikiwemo
rasilimali madini.
“Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ni Serikali inayowaangalia wanyonge.
Nimesikiliza kero zenu nitazifikisha na hatua itachukuliwa kwa mujibu wa
sheria. Mfanye subira," alisema Biteko
Aliongeza kuwa Serikali haipo tayari
kuona Watanzania wanyonge wanateseka na kwamba wakati umefika wa wao kunufaika.
Alifafanua kuwa suala lao
litashughulikiwa kwa wakati na kwa kuzingatia Sheria ili haki itendeke pasipo
kumuumiza yoyote.
Hata hivyo aliwakumbusha wananchi hao
kuhakikisha wanafuata utaratibu na sheria ili manufaa yapatikane bila kuleta
madhara yoyote.
Aidha, kwa mujibu wa Mthamini wa
Wilaya ya Shinyanga, Devotha Njella ni kwamba wananchi waliofanyiwa tathmini ni
500 na kwamba bado mwananchi mmoja mwenye heka 25 na nyumba 6 ambaye alikataa.
Alifafanua kwamba malipo hayo ya fidia
yalifanyika kwa awamu mbili na kwamba katika awamu ya kwanza Shilingi 953,194,050.75
zililipwa na awamu ya pili kiasi kilicholipwa ni Shilingi 472,413,686.32 na
kwamba bado kiasi cha Shilingi 208,886,951.01 ambacho taratibu za kulipa
zinaendelea.
No comments:
Post a Comment