Uingereza imetoa
mchango wa Shilingi Bilioni 6 kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuchangia
ujenzi wa miundombinu ya shule zilizopata madhara kufuatia tetemeko la ardhi
lililotokea katika Mkoa wa Kagera tarehe 10 Septemba, 2016.Mchango wa fedha hizo
umewasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli na Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Catherine Cooke, Ikulu
Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya Balozi huyo kuwasilisha hati zake za
utambulisho.
Balozi Sarah Catherine
Cooke amemueleza Rais Magufuli kuwa pamoja na kutoa mchango wa fedha hizo
Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May anatoa pole kwa Serikali ya Tanzania
na kwa familia zote zilizopatwa na madhara ya tetemeko hilo na kwamba Uingereza
imeona ishirikiane na Tanzania katika kukabiliana na madhara hayo.
“Uingereza imeguswa sana na maafa
yaliyowakumba wananchi kufuatia tetemeko lililotokea Kagera, tunapenda kuona
wananchi wanasaidiwa na wanafunzi wanaendelea na masomo” amesema Balozi Sarah Catherine Cooke.
Kwa Upande wake Rais
Magufuli amemshukuru Waziri Mkuu wa Uingereza kwa mchango huo ambao utasaidia
juhudi za Serikali za kuhakikisha inarejesha miundombinu iliyoharibika zikiwemo
shule.
“Mhe. Balozi Sarah Catherine Cooke naomba unifikishie shukrani zangu za
dhati kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May na umueleze kuwa kwa niaba
ya watanzania hususani waliopatwa na madhara ya tetemeko la ardhi tumeguswa
sana na moyo wake wa upendo kwetu” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli na
Balozi Sarah Catherine Cooke pia wamezungumzia uhusiano na ushirikiano mzuri
uliopo kati ya Tanzania na Uingereza ambapo Rais Magufuli ametoa wito kwa
Balozi huyo kuendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Uingereza
kuongeza uwekezaji wao hapa nchini na kwamba Tanzania itaendeleza na kukuza
uhusiano huo.
“Uingereza ni rafiki na ndugu wa kweli na wa kihistoria kwa Tanzania,
tunatambua kuwa nchi yenu ni mdau mkubwa na muhimu wa maendeleo yetu, hivyo
tusingependa kupoteza rafiki na ndugu yetu, tuendelee kushirikiana kwa manufaa
ya wananchi.
“Natambua kuwa Uingereza ina utaalamu mkubwa
katika masuala ya gesi hivyo nawakaribisha waje wawekeze katika sekta ya gesi”amesisitiza Rais
Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli
amesema Serikali itahakikisha fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya kusaidia
kukabiliana na madhara ya maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera
zinafikishwa kwa walengwa na ameonya kuwa watakaothubutu kuiba fedha hizo
watashughulikiwa.
Dkt. Magufuli
amebainisha kuwa baada ya kutengua uteuzi na kuchukua hatua nyingine dhidi ya
aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Amantius Msole na Mkurugenzi wa
Manispaa ya Bukoba Bw. Steven Makonda pamoja na kumsimamisha kazi Mhasibu Mkuu
wa Mkoa wa Kagera Bw. Simbaufoo Swai, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
CRDB Dkt. Charles Kimei awachukulie hatua watumishi wa Benki hiyo
walioshirikiana na watumishi hao kufanya njama za kuanzisha akaunti nyingine ya
benki yenye jina linalofanana na akaunti rasmi ya “Kamati ya Maafa Kagera” kwa
lengo la kujipatia fedha”
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Septemba, 2016
No comments:
Post a Comment