Mpaka kufikia 2021
serikali imeahidi kusambaza umeme wa kutosha na wa uhakika katika vijiji vyote
nchini ili kuendana na dhamira ya kuelekea katika uchumi wa kati kupitia
viwanda.
Hayo yamesemwa na
Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo wakati wa kipindi cha
TUNATEKELEZA kinachorushwa na Televisheni ya Taifa ya TBC1 kwa ushirikiano na
Idara ya Habari-MAELEZO.
Prof. Muhongo alisema
kuwa kukamilika kwa miradi ya kuzalisha nishati ya umeme ikiwemo Mradi wa
Kinyerezi 1 unaozalisha megawati 150 kwa siku umesaidia kuongeza upatikanaji wa
huduma ya umeme wa kutosha mijini na baadhi ya vijiji.
“serikali sasa ipo
katika kutekeleza miradi mikubwa ya nishati za umeme na gesi ikiwa ni jitihada
za kuhakikisha mpaka kufikia 2021 vijiji vyote nchini viwe vimepata huduma ya
nishati ya umeme”. Alisema Prof. Muhongo
Aidha, Prof. Muhongo
alisema kuwa utekelezaji wa Miradi hiyo unaenda sambamba na lengo la Serikali
ya awamu ya Tano ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo 2025.
Akizungumzia kuhusu
mikakati ya kuthibiti utoroshaji wa madini nchini Prof. Muhongo alisema kuwa
serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuwakamata watoroshaji wa
madini hasa katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege.
Prof. Muhungo alisema
kuwa kuanzia mwaka 2012 wamekamata madini ya aina mbalimbali zaidi ya Tani 10
yaliyokuwa yanatoroshwa kutoka nchini kwenda nchi mbalimbali.
Prof. Muhongo
amewataka watanzania kutumia fursa mbalimbali zitakazotokana na utekelezaji wa
miradi katika sekta ya gesi na mafuta ili kujiongezea kipato na kuiwezesha nchi
kutimiza malengo yake kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati.
No comments:
Post a Comment