Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mkandarasi
Nyanza Road Construction inayojenga barabara ya Furahisha hadi Pasiansi KM 2.8
wakati alipokagua ujenzi wa barabara hiyo, jijini Mwanza.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi wa kampuni
ya Beijing Construction Engineering Group anayejenga uwanja wa ndege wa Mwanza
kumaliza kazi ya upanuzi wa uwanja huo ifikapo mwezi Februari Mwakani.
Profesa Mbarawa ametoa
kauli hiyo alipokuwa akikagua kazi ya ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege wa
Mwanza pamoja na daraja la watembea kwa miguu lililopo maeneo ya furahisha,
jijini Mwanza.
Profesa Mbarawa
amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi na upanuzi wa uwanja huo kutaimarisha hali
ya usafiri wa anga kwa wakazi wa Mwanza na mikoa mingine na hivyo kukuza
shughuli za kibiashara nchini.
“Hakikisheni upanuzi wa uwanja wa ndege huu
unakamilika haraka ili kurahisisha na kuboresha huduma za usafirishaji
kiwanjani hapa”,alisema Waziri Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa
amemtaka mkandarasi wa kampuni ya Nyanza Road Construction kumaliza kwa wakati
upanuzi wa barabara ya ‘Mwanza-Airport’ eneo linaloanzia Ghana Quarters hadi
Uwanja wa Ndege wa Mwanza KM 9.15 pamoja na daraja la watembea kwa miguu la
furahisha ili kukuza uchumi na kupunguza kero ya msongamano wa magari katika
jiji la Mwanza.
Katika hatua nyingine
Prof. Mbarawa amewataka wananchi wa Mwanza kutoharibu miundombinu ya barabara
na madaraja ambayo Serikali inatumia gharama kubwa katika utengenezaji wake.
“Naomba muitunze na kuithamini miundombinu hii kwani Serikali inatumia
gharama kubwa katika kutengeneza na kukarabati”, alisisitiza Prof.
Mbarawa.
Ujenzi wa uwanja wa
ndege wa Mwanza ni mkakati wa Serikali kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo
unaboreshwa kuwa wa kisasa na wa kimataifa ili kuwezesha ndege kubwa kutua kwa
wingi na kuwa kiungo muhimu kwa mikoa 10 ya kanda ya Ziwa na Kati.
No comments:
Post a Comment