Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amepokea michango wa zaidi ya sh. bilioni 1.4 kutoka kwa mabalozi wa
nchi za nje nchini Tanzania na Jumuia ya Wafanyabiashara wa Kitanzania kwa
ajili ya kusaidia wananchi waliothirika na tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani
Kagera.
Akizungumza katika
hafla ya uchangishaji fedha kwa ajili ya kusaidia wahanga hao jana Jumanne, 13
Septemba, 2016 Waziri Mkuu aliwashukuru kwa michango yao ya fedha na vifaa vya
ujenzi ikiwemo mifuko 2,800 ya saruji. Amesema tetemeko hilo ni kubwa na
halijawahi kutokea nchini.
Alisema tetemeko hilo
limesababisha Serikali kuzifunga shule zake mbili za sekondari za Nyakato na
Ihungo kati ya nne zilizoathirika vibaya na tetemeko hilo.
“Serikali itajitahidi kuhakikisha inarejesha miundombini iliyoharibiwa
na tetemeko hilo katika kipindi kifupi ili wanafunzi na wananchi wengine waweze
kuendelea na shughuli zao za kawaida,” alisema.
Waziri Mkuu alisema
katika kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa haraka tayari Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista
Muhagama yuko mkoani Kagera akiongoza kitengo cha maafa kufanya thamnili kujua
athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.
Mawaziri wengine
walioko mkoani Kagera wakiendelea kufanya tathmini hiyo ni pamoja na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.
Alisema Kamati ya
Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa ya mkoa wa
Kagera imefungua akaunti maalumu katika benki ya CRDB kwa ajili ya kupokea
michango kutoka kwa watu mbalimbali. Namba za akaunti hiyo ya Kamati ya Maafa
ya Kagera ni CRDB 0152225617300.
Pia Waziri Mkuu
aliwapongeza na kuwashukuru waheshimiwa Wabunge kwa kuamua kutoa posho zao za
kikao cha jana kwa ajili ya kuchangia wahanga wa tetemeko hilo na kuwaomba
wananchi wengine kujitokeza na kutoa michango yao.
Wakati huo huo
viongozi wa makampuni ya mafuta ya GBP, Oil Com na Moil wameahidi kujenga shule
mbili za Nyakato na Ihungo ambazo sehemu kubwa ya miundombinu yake imeharibika
vibaya. Shule hizo zitajengwa katika kipindi cha siku 30.
Hafla hiyo
iliyoongozwa na Waziri Mkuu ilihudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara,
Charles Mwijage, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dk. Suzan Kolimba na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi, Dk. Aziz
Mlima.
No comments:
Post a Comment