Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amepokea jumla
ya sh. bilioni 1.040 kutoka kwa watumishi na wadau mbalimbali zikiwa ni misaada
kwa wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera
Septemba 10, mwaka huu.
Makabidhiano ya
michango hiyo, yamefanyika leo mchana (Jumanne, Septemba 20, 2016) kwenye
ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi hundi kwa
Waziri Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi alisema kiasi cha sh.
1,000,030,100 kimekusanywa kutoka kwa watumishi wa idara na Wizara zote
za Serikali na kwamba michango zaidi bado inaendelea kukusanywa.
“Tunaamini michango
hii itasaidia kuwafuta machozi wenzetu waliopatwa na maafa japokuwa tunajua
haitatosha kurudisha kile walichopoteza. Tuna imani itasaidia kupunguza makali
ya machungu waliyoyapata,” amesema.
Hata hicyo, Balozi
Kijazi amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba bado wanaendelea kukusanya michango
kutoka kwenye nyingine ambazo zilichelewa kupata taarifa na kwamba
wakikamilisha wataiwasilisha mapema iwezekanavyo.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amepokea michango ya sh. milioni 40 na kati ya hizo, sh. milioni 20
zimetolewa na kampuni ya ujenzi ya CHICO ya China na sh. milioni 20 nyingine
zimetoka kwa Umoja wa Wafanyabiashara na Wenye Viwanda wa India waliopo nchini
(India Business Forum).
Akiwasilisha mchango
wake, Mwakilishi Mkuu wa kampuni ya CHICO hapa nchini, Bw. Guo Zhijian alisema
wamesikitishwa na maafa yaliyotokea mkoani Kagera. “Tumefanya miradi mingi
mkoani Kagera ikiwemo ujenzi wa barabara za urefu kilometa 300, kwa hiyo mkoa
huu tunaujua zaidi. Tunatoa pole kwa wote waliopatwa na maafa hayo,”
amesema.
Naye Mwenyekiti wa
umoja wa wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka India (IBF), Bw. Gagan Gupta
alimweleza Waziri Mkuu kwamba wameshtushwa na tukio hilo na kwamba
wametanguliza kiasi hicho ili kisaidie juhudi za Serikali katika kukabiliana na
maafa hayo.
“Bado tunaendelea
kuwasiliana na wenzetu wengine na tukipata michango zaidi tutaiwasilisha mapema
iwezekanavyo,” amesema.
Akitoa shukrani kwa
waliotoa michango yote hiyo, Waziri Mkuu amewashukuru kwa misaada hiyo na
kuahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa
walengwa.
“Tunashukuru sana kwa
michango yote. Michango hii ni muhimu na inaonyesha mshikamano wa dhati uliopo.
Michango hii inaonyesha kuguswa na mapenzi ya dhati kwa waliopatwa na maafa.
Napenda niwahakikishie kuwa Kamati za Maafa za Mkoa, Ofisi ya Waziri Mkuu na kamati
za wilaya, ziko pale kuhakikisha walengwa wanafikiwa,” ameongeza.
Waziri Mkuu amesema
Serikali inakamilisha tathmini ya maafa hayo na kuahidi kutoa taarifa ya kiasi
kilichokusanywa na kiasi kilichotumika. Amewaomba wananchi waliotoa ahadi zao
za michango wakamilishe ahadi zao.
“Ninawaomba wale
walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi zao na wale walio mbali na benki
watumie namba za simu zilizotolewa mahsusi kwa ajili ya kuchangia maafa hayo,”
amesisitiza.
Akaunti ya maafa
imefunguliwa katika Benki ya CRDB yenye namba 015 222 561 7300 kwa jina la
KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz na namba za simu za mkononi
zinazotumika kupokea michango hiyo ni 0768-196-669 (M-Pesa) au 0682-950-009
(Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).
Tetemeko hilo
lililotokea Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu, lilisababisha vifo vya watu 17 na
wengine 440 kujeruhiwa. Kati yao, watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153
walilazwa, 113 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na matibabu
ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na wanaendelea vizuri.
Pia tetemeko hilo
limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali
hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi
126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM.
JUMANNE, SEPTEMBA 20,
2016.
No comments:
Post a Comment