Leo September 26 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli ametembelea Bandari ya Dar es Salaam na kuzungumza na
wafanyakazi wa bandari hiyo ambapo pamoja na mambo mengine ametoa miezi miwili
kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kununua mashine nne za kukagulia mizigo
bandarini (Scanning Mashine).
Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa kati ya
mashine nne za ukaguzi wa mizigo zilizopo, ni mashine mbili tu ndizo zinafanya
kazi na hazina uwezo wa kukagua mizigo yote inayotoka na kuingia nchini kupitia
bandari hiyo hali inayosababisha kutokuwepo kwa udhibiti wa uhakika wa
udanganyifu.
“Kwa hiyo nawaagiza TPA, na
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Mbarawa na Mamlaka ya Mapato
mpo hapa hakikisheni mnanunua mashine za kukagulia mizigo nne ndani ya miezi
miwili, na ikifika miezi mitano
muwe mmenunua mashine sita, ni lazima mizigo
yote ikaguliwe kwa mashine”
Dkt. Magufuli ameiagiza (TPA) kwa kushirikiana na Wizara husika
kuanza mazungumzo na kampuni ya kimataifa ya kuhudumia shehena ya makasha
bandarini (TICTS) ambayo inapakia na kupakua mizigo katika gati namba nane hadi
kumi na moja ili kurekebisha mkataba ambao Kampuni hiyo imeingia na Serikali
kwa lengo la kuhakikisha nchi inapata manufaa yanayostahili.
Rais Magufuli alitetembelea eneo la mita za kupimia mafuta
yanayopakuliwa melini (Flow Meters) na kubaini kuwa mita hizo hazifanyi kazi,
ameiagiza TPA kuharakisha mchakato wa kununua mita mpya na kuzifunga katika
eneo hilo ili kudhibiti ukusanyaji wa mapato ya kodi ya mafuta.
Aidha, Dkt. Magufuli ameitaka TPA kujipanga kujenga bandari kavu
(ICD) katika eneo la Ruvu Mkoani Pwani ili kuachana na bandari kavu zilizoanzishwa
na watu binafsi hapa Jijini Dar es Salaam na ambazo zimekuwa zikitumika kukwepa
kodi.
No comments:
Post a Comment