Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameridhia na kusaini Miswada
mitano kutumika kama Sheria kamili za nchi.
Hayo yamesemwa na
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai mara baada ya
kufungua Mkutano wa nne wa Bunge la 11 leo mjini Dodoma.
Miswada
iliyoidhinishwa na Rais ni pamoja Sheria ya Fedha na Matumizi ya mwaka 2016,
Sheria ya Fedha namba 2 ya mwaka 2016, Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali ya mwaka 2016, Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbambali namba 2 na 4
ya mwaka 2016 na Sheria ya Marekebisho ya Ununuzi ya Umma namba 5 ya mwaka
2016.
Aidha, Mhe. Spika
amewakumbusha Wabunge kusoma na kuelewa kila kinachokuja Bungeni ili waweze
kutekeleza majukumu yao ya kibunge ipasavyo kwa niaba ya wananchi waliowatuma
kufanya kazi hiyo ili kuwaletea maendeleo.
Wabunge wametakiwa
kutekeleza majukumu hayo ya uwakilishi wa wananchi ili waweze kujadili masuala
mbalimbali kwa kuzingatia haki, ustahimilivu, busara, hekima na kutumia lugha
ya staha katika mijadala ya Bunge.
Vile vile Mhe. Spika
amempongeza Naibu Spika Dkt. Tulia Akson kuongoza vema mkutano wa tatu wa Bunge
ulioanza Aprili 19 na kumalizika Juni 30 mwaka huu kwa kushirikiana na
wenyeviti wa Bunge Andrew Chenge, Mussa A. Zungu na Najima Giga.
Katika hatua nyingine
Mhe. Spika amemshukuru Rais Dkt. Magufuli, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Watanzania wote walimuombea alipokuwa kwenye matibabu
nje ya nchi pamoja na Madaktari waliomhudumia akiwa kwenye matibabu na
kumshukuru Mungu kwa kumwonesha upendo alipokuwa kwenye mapito ya kuugua.
Katika mkutano huo wa
Bunge yameulizwa maswali 14 ambayo yalielekezwa kwenye Wizara mbalimbali na
kujibiwa kwa llengo la kutolea ufafanuzi masuala yanayotekelezwa kwa Serikali.
No comments:
Post a Comment