Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Pombe
Magufuli, leo tarehe 19 Septemba, 2016 amefanya ziara ya kushitukiza katika
Ofisi za Gazeti la Uhuru zilizopo Mtaa wa Lumumba Jijini Dar es Salaam na kuzungumza
na wafanyakazi.
Katika Mazungumzo
hayo, wafanyakazi wa Gazeti la Uhuru linalomilikiwa na CCM wamelalamikia
kutolipwa mishahara yao kwa miezi saba, kutotolewa kwa michango ya wafanyakazi
kwa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kuuzwa kwa mtambo wa kuchapisha
magazeti katika hali ya kutatanisha, kutotambuliwa katika ajira kwa baadhi ya
wafanyakazi, kutolipwa kwa madeni wanayozidai taasisi za Serikali na
wanaostaafu kutolipwa mafao yao.
Wafanyakazi hao pia
wamemueleza Dkt. Magufuli kuwa Bodi na Menejimenti ya kampuni ya vyombo vya
habari vya chama inayoendesha Gazeti la Uhuru na Redio Uhuru zimeshindwa
kuendesha vyombo hivyo na wamemuomba aingilie kati ili kuvinusuru vyombo hivyo
ambavyo kwa sasa vina hali mbaya kutokana na kukabiliwa na madeni makubwa, na
biashara yake imeshuka kwa kiasi kikubwa.
Akijibu malalamiko
hayo Rais Magufuli aliyetembelea ofisi za Gazeti la Uhuru akitokea Ofisini
kwake katika jengo la Makao Makuu ya chama, Ofisi Ndogo ya Lumumba Jijini Dar
es Salaam amemuagiza Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Abdulrahaman Kinana kuhakikisha
mishahara yote wanayodai wafanyakazi inayofikia Shilingi Milioni 609 inalipwa
ndani ya Mwezi huu wa Tisa, ameagiza kupatiwa orodha ya taasisi za Serikali
zinazodaiwa na Magazeti ya Uhuru na Mzalendo, na pia ameagiza deni linalodaiwa
na NSSF kutokana na kutowasilishwa kwa makato ya wafanyakazi lilipwe.
Kuhusu malalamiko
dhidi ya Bodi na Menejimenti ya Kampuni hiyo, ajira za wafanyakazi, mafao kwa
wastaafu, kuuzwa kwa mtambo wa kuchapisha magazeti na mazingira magumu ya kazi
Dkt. Magufuli ameahidi kuyafanyia kazi.
Aidha, Dkt. Magufuli
amewapongeza wafanyakazi wa Gazeti la Uhuru kwa kazi kubwa na nzuri
wanayoifanya licha ya kukabiliwa na changamoto kubwa na amewakikishia kuwa
anatambua umuhimu wao na kwamba atahakikishia anaboresha hali ya chombo hicho
muhimu.
Wakati huo huo, Rais
Magufuli amemjulia hali Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samwel Sitta ambaye anaendelea kupata matibabu Jijini Dar es
Salaam na hali yake inaendelea vizuri.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Septemba,
2016
No comments:
Post a Comment