Wananchi wameaswa kuwa
wavumilivu na kuendelea kushirikiana na Serikali wakati jitihada mbalimbali
zikiendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za tetemeko la ardhi
lililotokea Mkoani Kagera hivi karibuni.
Hayo yamesemwa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) George Simbachawene alipokuwa akitoa
kauli ya Serikali bungeni kuhusu Maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi
lililotokea Mkoani Kagera siku ya jumamosi tarehe 10/09/2016.
Waziri Simbachawene
amesema kuwa hadi leo tarehe 13/9/2016 idadi ya vifo vilivyosababishwa na
tetemeko hilo katika Mkoa wa Kagera ni 17, ambapo majeruhi waliolazwa katika
hospitali mbalimbali zilizoko Mkoani humo ni 169, majeruhi waliotibiwa na
kuruhusiwa ni 83, nyumba za makazi zilizoanguka ni 840, nyumba za makazi zenye
nyufa ni 1,264 pamoja na taasisi zilizoanguka na kupata nyufa ni 44.
Aidha, Waziri
Simbachawene amesema kuwa mpaka sasa Serikali imechukua hatua za kuwaokoa watu
na kuwapeleka hospitali kwa ajili ya matibabu na kuwapatia makazi ya muda
baadhi ya wananchi ambao nyumba zao zimeathirika.
Pia Serikali
inaendelea kutibu majeruhi bure na wenye Bima za Afya kutumia bima zao na
kuongeza nguvu ya madaktari bingwa 15 kutoka mkoa ya Mwanza ili kuweza kutoa
huduma ya haraka kwa wahanga hao.
Vilevile Waziri
Simbachawene amesema kuwa Serikali imeelekeza wanajiolojia kuwatoa hofu
wananchi kwa kutoa maelekezo ya kisayansi kuhusu hali hiyo na kuendelea kufanya
tahimini ya athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.
Hata hivyo Waziri
Simbachawene amesema kuwa serikali imezifunga shule za sekondari Ihungo na
Nyakato zilizopo mkoani humo kutokana na athari za tetemeko iliyopelekea
kuharibika kwa miundombinu ikiwemo madarasa, vyoo, mabweni na maabara, wakati
serikali ikiendelea na taratibu za kushughulikia tatizo hilo.
Waziri Simbachawene
ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa hatua za dharura
zinachukuliwa kwa kushirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha ili kuwasaidia
wahanga.
Mbali na hayo Mbunge
wa Mlalo Mhe. Rashid Shangazi ametoa hoja juu ya wabunge kuchangia posho yao ya
siku moja ili iweze kuwasaidia wahanga wa tetemeko hilo lililokadiriwa kuwa na
ukubwa wa kiwango cha 5.7 katika vipimo vya Richter ambapo wabunge waliunga
mkono hoja hiyo na kuridhia kuchangia kusaidia maafa hayo.
Aidha, Mbunge wa
Muleba, Prof. Anna Tibaijuka ameishukuru Serikali kuwepo kwenye eneo la tukio
mkoani Bukoba hatua ambayo imewapa faraja wanakagera na kutoa wito kwa wabunge
na watu wenye mapenzi mema kuzidi kuwafariji wahanga hao.
Kwa upande wake Waziri
wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Charles Tizeba amesema kuwa Serikali itafanya
tathmini ya kina na ya kitaalamu ili kuepuka wale ambao wanatumia maafa hayo
katika kujinufaisha.
Akishukuru kwa niaba
ya Serikali Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
amewashukuru wadau wote kwa kujitokeza na kushirikiana na Serikali katika
kutatua changamoto na kuwahakikishia wabunge kuwa mchango wao utawafika
walengwa na kuongeza kuwa jambo hilo limepelekea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kusitisha safari yake nchini Zambia ili kuweza kusimamia suala hilo.
Aidha, Waziri Lukuvi
amesema kuwa Serikali inauchungu mkubwa juu ya maafa hayo, hivyo amewataka
wadau mbalimbali kujitokeza kusaidiana na Serikali ili kuweza kuwasaidia
wahanga hao na kuwapa pole waathirika wa tetemeko hilo na kuwaombea
marehemu wapumnzike kwa amani.
No comments:
Post a Comment