Ajali hiyo imetokea siku mbili baada ya ile ya basi la Kampuni
ya New force iliyotokea mkoani Njombe ikihusisha basi lenye namba T 429
DEU lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Songea mkoani Ruvuma, ambapo watu
12 walifariki dunia na wengine 28 kujeruhiwa vibaya. Katika ajali ya Mwanza,
gari dogo aina ya Hiace liligongana uso kwa uso na basi la Super Shem na
kusababisha vifo hivyo na wengine 10 kujeruhi.
Ajali hiyo imetokea umbali wa mita 200 kutoka kituo kidogo cha
mabasi cha Hungumalwa njia panda ya Shelui na Mwamashimba katika Kijiji cha
Mwamaya wilayani Kwimba mkoani Mwanza. Ilielezwa katika tukio hilo, dereva wa
Hiace aliingia barabara kuu ya Mwanza-Shinyanga bila kuchukua hadhari na hivyo
kukutana na basi hilo.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Ahmed Msangi alisema baada ya ajali hiyo watu 10 walikufa papo hapo na
wengine 11 kujeruhiwa, ambapo mmoja alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa
Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na wawili walifariki dunia wakati wakipelekwa
Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa matibabu zaidi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, Dk. Bethod
Nchemba, akizungumzia ajali hiyo alisema walipokea majeruhi 10
wakiwemo wanaume na wanawake watano ambapo mmmoja alikuwa na hali mbaya
na alifariki akiwa mapokezi wakati akiendelea kupewa huduma.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Monica Shija, Christina
Costantine, Theresia Majenga wote wakiwa wakazi wa Kijiji cha Gulumwa wilayani
Kwimba, Lwinzi Kope mkazi wa Kijiji cha Chaselwe, Mabula Magi wa Rukwa, Isaya
Deogratius mkazi wa Mbande, Moses Kamel wa Kijiji cha Bupamwadomu, George Ndila
mkazi wa Sangu, Kondakta wa hiace aliyefahamika kwa jina moja la Poni pamoja na
mtu mmoja mwanaume, mama mmoja na mtoto ambao hawajafahamika wote wakiwa ni
abira wa Hiace.
Alisema majeruhi watatu wanaendelea vizuri na matibabu
katika hospitali hiyo na miili tisa kati ya 11 imeshatambuliwa isipokuwa mwili
wa mama mmoja na mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 5 na majeruhi sita
wamelazimika kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.
No comments:
Post a Comment