Timu ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara (The Kilimanjaro Qeens) imetwaa kombe la Challenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, baada ya kuifunga Kenya, mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliopigwa leo Jinja , nchini Uganda.
Kwa matokeo hayo, Kilimanjaro Qeens wanakuwa ndiyo
mabingwa wa kwanza na wa kihistoria wa michuano hiyo ambayo ni mipya kabisa
kuanzishwa katika ukanda ukanda wa Afrika Mashariki chini ya baraza lake la
CECAFA.
Mabao ya timu ya taifa Tanzania
ya wanawake maarufu kama Kilimanjaro Queens katika mchezo wa leo Septemba 20,
2016 yamefungwa na Mwanahamisi Omari katika kipindi cha kwanza kabla ya Kenya
kujitutumua na kupata bao la kufutia machozi kipindi cha pili katika mchezo
uliokuwa na ushindani wa aina yake.
Kilimanjaro Queens iliingia
fainali baada ya ushindi wa 4-1 dhidi ya wenyeji, Uganda, wakati Kenya
iliifunga 3-2 Ethiopia ambapo Tanzania Bara iliongoza Kundi B baada ya kushinda
kura ya sarafu kufuatia sare ya 0-0 na Ethiopia katika mchezo wa mwisho wa kundi
hilo, hivyo kufungana nayo kwa pointi na wasatani wa mabao kileleni.
Kilimanjaro Queens ilianza vizuri
michuano hiyo kwa kuibamiza 3-2 Rwanda, mabao yake yakifungwa na Asha Rashid
‘Mwalala’ dakika za 11 na 65 na Stumai Abdallah dakika ya 28, wakati ya wapinzani
wao yalifungwa na Ibangarrue Marie na Amina Ally wa Tanzania Bara aliyejifunga.
Afisa habari wa Shirikisho la
Soka Tanzania TFF, Alfred Lucas, amesema timu hiyo inaondoka Uganda leo, na
itapitia mkoani Kagera ambako itakaa kwa siku moja kwa ajili ya kuwafariji
waathirika wa tetemeko la ardhi, na kisha kesho kutwa itawasili jijini Dar es
Salaam, ikiwa na kombe lake, na kwamba utaratibu wa mapokezi unaandaliwa.
Kwa niaba ya TFF, Lucas
ameipongeza timu hiyo, na kuwaahidi wapenzi wa soka nchini makubwa zaidi.
No comments:
Post a Comment