Tetemeko la ukubwa wa mtikisiko wa
kipimo cha Ritcher 5.7 limetokea katika mikoa mitatu nchini na watu zaidi ya 10
wamekufa na wengine 120 wamejeruhiwa huku majengo mengi yakibomoka.
Mikoa iliyoripotiwa
kuathiriwa kwa tetemeko hilo ni Kagera, Mwanza na Mara. Pia tetemeko hilo
limeukumba mji wa Kampala na Rakai nchini Uganda jana saa 9.27 alasiri.
Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema tetemeko hilo limetokea saa tisa
alasiri na zaidi ya watu 10 wamekufa.
Awali, akizungumza kwa
simu kutoka jiijini Dar es Salaam, Kamanda Ollomi alisema watu wanane walikufa
na baadaye alisema idadi hiyo iliongezeka na kwamba alipata taarifa kutoka
hospitali ya mkoa kuwa wamepokea miili ya watu 10 na wameihifadhi.
Alisema tisa kati ya
waliokufa ni wakazi wa Manispaa ya Bukoba na mmoja ni mkazi wa wilayani
Karagwe.
Kamanda alisema
miongoni mwa majeruhi wamo wanafunzi 15 wa Shule ya Sekondari ya Wavulana
Ihungo na wapo katika hospitali ya mkoa wanaendelea kupatiwa huduma. Alisema
bado vikosi vya uokoaji likiwemo Jeshi la Polisi na Zimamoto vinaendelea na
uokoaji.
Alisema watu
waliojeruhiwa na waliokufa wamedondokewa na kuta, vifusi na vyombo vya ndani.
Alisema wengine
walikufa kwa mshituko unaosababishwa na shinikizo la damu na nyumba zaidi ya 40
zimeathirika.
“Ni kweli tetemeko la
ardhi limetokea na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za watu, vifo pamoja na
majeruhi na bado tunaendelea kupokea taarifa zaidi,” alisema Kamanda
Ollomi na kuongeza kuwa mpaka jana jioni walikuwa wakiendelea kupokea taarifa
kutoka sehemu mbalimbali za mkoa huo kuhusu vifo na majeruhi.
Wakala wa Jiolojia
waelezea ukubwa wake
Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Profesa Abdulkarim Mruma alisema tetemeko
hilo ni kubwa kwa nusu ya kipimo cha juu cha Ritcher10 na limezidi kipimo cha
chini cha ukubwa wa Ritcher tatu. Alisema limezidi lililotokea Dodoma hivi
karibuni.
Profesa Mruma alisema
tetemeko hilo limetokea katika mpaka wa Tanzania na Uganda, kilometa 47
kaskazini mwa Bukoba mkoani Kagera na sababu ni mpasuko wa ardhi katika Bonde
la Ufa la magharibi karibu kabisa na Ziwa Victoria .
Amewataka wananchi
kuchukua tahadhari kwani kwa kawaida linapotokea tetemeko kubwa kama hilo hufuatiwa
na matetemeko madogo na ardhi hutulia baada ya siku mbili mpaka tatu.
“Kwa wakati huu ili kuepuka madhara zaidi, litakapotokea watoke nje ya
nyumba na kukaa mbali na miti kwenye uwanja wa wazi na wanaoendesha magari
waache mara moja,” alisema Profesa Mruma.
Alisema kwa sasa
wataalamu katika kituo chao cha kupimia matetemeko cha Geita wanaendelea kupata
takwimu zaidi kutokana na kuwa mpasuko wa tetemeko hilo umekuwa karibu sana na
ziwa Victoria na baadaye watatoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa undani.
No comments:
Post a Comment