Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 7 kwa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kulipa deni la bilioni 2 ambalo wanadaiwa na
Shirika la nyumba la Taifa (NHC).
Dkt. Magufuli ametoa
agizo hilo kwa Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Injinia Joseph Nyamhanga leo
jijini Dar es Salaam katika ziara ya kushtukiza ya kuangalia ujenzi wa hosteli
za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Nawapa siku 7 muwe
mmelilipa hilo deni huku mkiendelea na utaratibu wa kuhamia Dodoma, kama
hamtalilipa kwa wakati nitawaagiza NHC kuwatolea vitu vyenu nje kama
wanavyofanya kwa wengine,” alisema Dkt. Magufuli.
Amesema kuwa kiwango
hicho cha bilioni 2 kingeiwezesha wizara hiyo kujenga ofisi za wizara kwa
kuwatumia Wakala wa Majengo (TBA) ambao wako chini ya wizara hiyo badala ya
kutumika kama kodi ya pango.
Aidha, ameitaka wizara
hiyo kuhamia Mjini Dodoma mara tu watakapokamilisha deni hilo na kutoendelea
kupanga jijini Dar es Salaam, kwani hakuna sababu ya kuendelea kupanga majengo
ya ofisi Dar es Salaam wakati Serikali yote inahamia Dodoma.
Wakati huohuo, Rais
Dkt. Magufuli ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Tecknolojia, Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wakala wa Majengo (TBA) na
uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kusimamia vizuri mradi wa
ujenzi wa hosteli za chuo kikuu ambao Rais mwenyewe aliahidi shilingi bilioni
10 katika ujenzi huo, bilioni 5 imekwishatolewa na bilioni nyingine 5 itatolewa
ndani ya wiki hii.
Hosteli hizo
zinategemea kuchukua wanafunzi 4000 ambapo itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo
la wanafunzi kukaa nje ya maeneo ya chuo.
No comments:
Post a Comment