Simba SC imekwama leo, baada ya kuambulia
sare ya 0-0 mbele ya wenyeji Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Matokeo hayo yanaiongezea pointi moja Simba
ikifikisha pointi 62 pamoja na zile tatu za mezani walizopewa kwa madai
Mohammed Fakhi alicheza akiwa ana kadi tatu za njano baada ya kufungwa na
Kagera Suagr 2-1.
Maana yake Simba SC inaendelea kuongoza Ligi
Kuu kwa pointi sita zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC ambao hata hivyo wana
mechi mbili mkononi.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Jacob
Adongo wa Mara, aliyesadiwa na Hassan Zani wa Arusha na Abdallah Mkomwa wa
Pwani dakika 45 za kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu.
Kulikuwa na kosa kosa pande zote mbili upande
wa Simba Muivory Coast, Frederick Blagnon akipoteza nafasi ya wazi na kwa Toto,
Nahodha Reliant Lusajo Mwakasagule naye akipoteza.
Kipindi cha pili kocha Mcameroon wa Simba,
Joseph Omog alianza kwa mabadiliko mfululizo akiwatoa kiungo Mohammed ‘Mo’
Ibrahim na mshambuliaji Laudit Mavugo na kuwaingiza kiungo Mwinyi Kazimoto na
mshambuliaji Ibrahim Hajib.
Pamoja na mabadiliko hayo, mchezo uliendelea
kuwa mgumu na Omog akaamua kumtoa na winga Shiza Ramadhani Kichuya na
kumuingiza mshambuliaji Juma Luizio Ndanda, wakati kocha wa Toto, Furgence
Novatus alimtoa Jamal Soud Mtengeta na kumuingiza Hamad Nathaniel Mbumba.
Bado mashambulizi yalikuwa ya pande zote
mbili na refa Adongo akaongeza dakika tano kufidia muda uliopotezwa. Toto
inafikisha pointi 26 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya 14 ikiishusha Maji Maji
nafasi ya 15.
Kikosi cha Toto Africans leo kilikuwa; Mwasa
Kirungi, Juvenary Pastory, Ramadhani Malima, Hamim Abdul, Yussuf Mlipili,
Carlos Kirenge, Jamal Mtengeta/Hamad Mbumba dk75, Hussein Kasanga, Waziri
Junior, Reliant Lusajo na Jaffar Mohammed.
Simba SC; Daniel Agyei, Janvier Besala Bokungu,
Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Juuko Murshid, James Kotei,
Shiza Kichuya/Juma Luizio dk76, Muzamil Yassin, Frederick Blagnon, Laudit
Mavugo/Ibrahim Hajib dk58 na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Mwinyi Kazimoto dk54.
No comments:
Post a Comment