Naibu Waziri wa Afya
Maendeleo ya Jamii Jinsi Wazee na Watoto Mhe. Dkt Hamisi Kigwangalla akijibu
hoja mbalimbali za wabunge katika kikao cha kwanza cha Mkutano wa saba wa Bunge
la 11 Mjini Dodoma
Serikali imeendelea
kuchukua hatua kwa kuendelea kutoa elimu katika Halmashauri za Wilaya, Manispaa
na Miji 72 ili kuondokana na tatizo la ndoa za utotoni zinazobababisha watoto
kukosa haki ya msingi ya kupata elimu.
Akijibu swali la Mhe.
Anna Kilango Malecela Mbunge wa Viti Maalum (CCM) lililouliza Je, Serikali ina
Mkakati gani wa kutokomeza ndoa za utotoni? Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya
Jamii Jinsi Wazee na Watoto Mhe. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa msisitizo
utazidi kuwekwa katika utoaji wa elimu kwa familia, wazee wa mila na jamii kwa
ujumla.
“Tutajikita kutoa
elimu zaidi ili jamii iachane na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati za
kuoza watoto wa kike” alisisitiza Mhe. Dkt. Kigwangalla.
Ameongeza kuwa
Serikali inatambua athari kubwa zinazosababishwa na ndoa za utotoni katika
jamii ya watanzania na itaongeza nguvu katika kutoa elimu na kupambana na wale
wote watakaojihusisha kwa namna moja au nyingine kuwanyima watoto wa kike haki
yao ya kupata elimu.
Aidha kulingana na
takwimu za Afya na Idadi ya Watu nchini za mwaka 2016 ndoa za utotoni
zimeshamiri katika mikoa ya Shinyanga kwa asilimia 59, Tabora kwa asilimia 58,
Mara kwa asilimia 55 na Dodoma kwa asilimia 51 hivyo Serikali itaendelea
kupambana kutokomeza ndoa za utotoni nchini.
Kwa upande wa muundo
wa kisera na kisheria, Serikali imezifanyia maboresho Sera na Sheria ili
kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa na mimba za utotoni pamoja na marekebisho
ya Sheria ya Elimu Sura 353 ambayo inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka
30 kwa mtu yoyote atakayempa mimba mwananfunzi wa shule ya Msingi au Sekondari.
Katika kutokomeza ndoa
na mimba za utotoni Serikali itaanza utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa
kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto mwezi June 2017 unaojumuisha Sekta
zote zinazohusu wanawake na watoto kwa lengo la kutokomeza aina zote za ukatili
na kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 47 hadi 10 ifikapo mwaka 2020.
No comments:
Post a Comment