Monday 24 April 2017

SERIKALI YAONDOA TOZO ZISIZO ZA LAZIMA KATIKA ZAO LA KOROSHO



Serikali kupitia Wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvivu imesema imeshughulikia malalamiko  ya wakulima wa Korosho kwa kuondoa makato yasiyokuwa muhimu katika zao hilo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Wizara hiyo Mhe.William Ole Nasha wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge leo Mjini Dodoma.

“Serikali imekwisha fanyia marekebisho maeneo ambayo wakulima walikuwa wanalalamikia kwa kuondoa kabisa makato hayo katika zao hilo”, Aliongeza Mhe.Ole Nasha.

Amesema kuwa Serikali imefuta ushuru wa shilingi 20 kwa kilo kwa ajili ya chama kikuu cha Ushirika,Shilingi 50 za usafirishaji wa Korosho,Shilingi 10 kwa kilo ajili ya mtunza ghala na pia shilingi 10 kwa kilo kwa ajili ya kikosi kazi cha Masoko.Aidha Sekta ina utaratibu maalum wa kupanga bei dira kwa kutumia vigezo vinavyokubaliwa kwa pamoja na wadau wote.

Kwa upande wa manunuzi ya pembejeo za korosho amesema hufanywa kwa pamoja na vyombo rasmi ndani ya Tasnia ambapo awali ilikuwa ikisimamiwa na mfuko wa Maendeleo ya Korosho na sasa Bodi ya korosho Tanzania.

Aidha ameeleza changamoto zinazojitokeza katika kufikisha pembejeo hizo kwa wakulima wa korosho na hatua zimechukuliwa kwa kushirikisha vyama vya ushirika ili kudhibiti mianya ya pembejeo kwenda kwa wasio lengwa.

Pia Serikali imeweka mfumo wa usambazaji wa pembejeo wenye lengo la kuhakikisha kwamba pembejeo hizo zinawafikia walengwa pekee.


“Utaratibu huu unazingatia kutambua wakulima wenye uhitaji na pembejeo na hununuliwa kwa kutumia utaratibu wa ununuzi wa pamoja n akusambazwa kwa wakulima kwa kutumia wakala  walioteuliwa na kudhibitishwa na Halmashauri husika”,Alisisitiza Mhe.Ole Nasha.

No comments:

Post a Comment