Monday, 24 April 2017

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA UCHUNGUZI WA MAGONJWA



Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imeanza hatua za awali za uainishaji wa gharama,uandaaji wa mfumo mbadala na upembuzi wa kina wa aina ya ubia ili kushirikiana na Sekta binafsi katika utoaji wa huduma za uchunguzi wa magonjwa.
Hayo yamesemwa leo bungeni na Naibu Waziri, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe.Hamis Kigwangalla wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge Mjini Dodoma.

“Kufuatia kukua kwa kasi kwa Sayansi na Teknolojia ya uchunguzi wa magonjwa,Wizara inakubaliana na wazo hili juu ya kuangalia namna nzuri ya kushirikiana na sekta binafsi katika utoaji wa huduma hizi,”Alisema Mhe.Kigwangalla.

Amesema kwa kuanzia sasa Wizara yake inafikiria kuanzisha ushirikiano kwa kupitia ukodishaji wa vifaa ambapo Serikali itakodisha mashine hizo ambazo zitakuwa za mbia na Serikali haitahusika na ununuzi,ufungaji na matengenezo kinga ya mashine hizo.

Aidha amebainisha kuwa katika mfumo huo,Wizara itakuwa na jukumu la kusimamia utoaji wa huduma na itapata gawio lake kutokana na makusanyo yatokanayo na uchangiaji wa huduma kulingana na mkataba.


“Ni imani ya Wizara kuwa kutumia mfumo wa ubia na sekta binafsi(PPP) huduma za uchunguzi wa magonjwa zitaimarika na kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama”,Aliongeza Mhe.Kigwangalla.

No comments:

Post a Comment