Tuesday, 11 April 2017

SERIKALI YAANDAA MUSWADA WA SHERIA KUSIMAMIA NA KUDHIBITI BIASHARA YA VYUMA CHAKAVU




Waziri wa Viwanda , Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage akijibu hoja mbalimbali za wabunge katika kikao cha tano cha mkutano wa saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeandaa Rasimu ya Muswada wa Sheria itakayoweka bayana taratibu na mfumo wa usimamizi na udhibiti wa bishara ya chuma chakavu katika hatua mbalimbali za uzalishaji, ukusanyaji, usambazaji, uuzaji na uyeyushaji wake kwa kuzingatia uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa manufaa ya Taifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge Mjini Dodoma.

“Biashara ya Chuma chakavu imeshamiri hapa nchini na duniani kwa ujumla,na hili limetokana na mahitaji ya vyuma chakavu ambapo kumetumiwa na wahalifu kuaharibu miundombinu iliyojengwa kwa vyuma kwa nia ya kupata chuma ili waiuze kama chuma chakavu”Alisema Mwijage.

Amesema ili kukabiliana na hujuma hizi Mamlaka husika zikiwemo TANESCO, TANROADS  na  RAHACO wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na jeshi la Polisi ikiwemo kutumia walinzi wa Taasisi husika ili kulinda rasilimali hizo.

Amesisitiza kuwa Muswada huu umeweka wazi na bayana adhabu itakayotolewa kwa mtu atakayebainika kuharibu miundombinu.
Aidha Mhe.Mwijage ametoa wito kwa watanzania kutoa taarifa pindi waonapo mtu anayehujumu  miundombinu kwa namna yote ile.


“Natoa wito kwa wenye viwanda na wafanyabiashara wa vyuma chakavu jiepusheni na ununuzi wa vyuma  ambavyo asili yake ina mashaka na tutaharakisha sheria  hii ili kutatua tatizo hili”Aliongeza Mwijage.

No comments:

Post a Comment