Kazi ya ujenzi wa
laini mpya ya umeme wenye nguvu ya 33KV kutoka Chalinze (Sub-station) kwenda
Mlandizi yenye urefu wa kilomita 45 kwa lengo la kuongeza umeme ili kukidhi
mahitaji ya upanuzi wa mtambo uliofanyika na kuweza kusukuma ujazo wa lita za
maji milioni 196 kwa siku sasa umekamilika na majaribio ya matumizi ya
laini hiyo yameanza kwa matarajio ya kukamilisha kazi hiyo ndani ya siku mbili.
Taarifa ya Mamlaka ya
Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) ilifafanua kwamba, DAWASA kupitia
Mkandarasi wake M/s WABAG kutoka nchini India kwa kushirikiana na Mkandarasi
Msaidizi, Kampuni ya M/s Mollel Electrical Contractors ya hapa
nchini kwa sasa wamemaliza kazi zote za ujenzi wa laini kutoka Chalinze
mpaka eneo la kuingizia umeme ndani ya Mtambo wa Maji wa Ruvu Juu uliopo
Mlandizi tayari kwa majaribio ya awali ya kiusalama na kuwasha pampu.
Mtambo huo wa maji wa
Ruvu Juu utakua ukipokea umeme wa kutosha kutoka katika transfoma kubwa iliyopo
kituo kidogo cha umeme Chalinze (Sub-station) yenye uwezo wa 45/55 MVA ambapo
itawezesha pampu zote mpya zilizofungwa kuwashwa.
Hapo awali mtambo huo
ulikuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 82 kwa siku na mara baada ya
majaribio haya na kuongeza umeme ndani ya siku mbili uzalishaji wake
utaongezeka kufikia lita milioni 196 kwa siku.
Taarifa ya DAWASA
inabainisha kuwa, ili lita hizo milioni 196 za maji ziweze kusukumwa na mtambo
huo wa Ruvu Juu, mtambo unahitaji 16MVA za umeme ili kusukuma maji safi
yanayozalishwa baada ya upanuzi kwa asilimia100.
Aidha, Mkandarasi kwa
sasa amekamilisha kazi ya kujenga laini hiyo mpya toka sub-station ya Chalinze
ikiwa ni pamoja na kazi zote zilizotakiwa kufanyika ndani ya kituo hicho kidogo
cha umeme cha Chalinze. Hizo ni pamoja na kazi mbalimbali zilizotakiwa
kufanyika ili kuweza kuupokea umeme huo kutoka kwenye transfoma hiyo.
Aidha, maeneo nufaika
ya mtambo wa maji wa Ruvu Juu ni Mkoa wa Dar es Salaam, mkoa wa Pwani, maeneo
ya mji wa Mlandizi, Kibaha na baadhi ya Vitongoji vyake.
DAWASA inaendelea
kulishukuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ushirikiano na ushauri wa
kitaalam kuhusiana na masuala ya umeme ambao imekua ikiutoa mara kwa mara ili
kuhakikisha kuwa maji ya kutosha yanapatikana katika jiji la Dar es Salaam na
maeneo yote yanayohudumiwa na DAWASA.
Mikataba ya upanuzi wa
mtambo na ujenzi wa mabomba mapya kutoka Ruvu Juu mpaka Kimara pamoja na ujenzi
wa tanki kubwa lenye ujazo wa lita million 10 ilisainiwa mwaka 2014 na Serikali
kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji ilipata fedha hizo kwa mkopo wa masharti
nafuu toka Benki ya Exim ya India.
No comments:
Post a Comment