Thursday, 25 August 2016

SAMATTA AWANIA TIKETI YA MAKUNDI EUROPA LEAGUE LEO


MSHAMBULIAJI wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Ally Samatta leo anatarajaiwa kuiongoza timu yake katika mchezo wa marudiano hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Europa League dhidi ya Lokomotiva Zagreb ya Croatia Uwanja wa Luminus Arena, Genk.
Nahodha huyo wa Tanzania, Alhamisi iliyopita alifunga bao moja KRC Genk ikitoa sare ya 2-2 dhidi ya Lokomotiva Zagreb Uwanja wa Maksimir mjini Zagreb, Croatia katika mchezo wa kwanza na kesho pia katika mchezo wa marudiano nyumbani, Samatta amepania kufanya makubwa.


Akizungumza  kutoka Genk juzi, Samatta alisema kwamba anamshukuru Mungu wanakwenda katika mchezo wa marudiano wakitoka kushinda 3-0 katika Ligi ya Ubelgiji. 
Samatta aliyeendeleza moto wake wa mabao kwa kufunga mabao mawili Genk ikishinda 3-0 dhidi ya wenyeji, Lokeren Uwanja wa Daknamstadion mjini Lokeren Jumapili katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji, alisema wataingia kwenye mchezo wa kesho kwa lengo la kushinda.
Samatta alifunga mabao yote mawili ya mwanzo Jumapili, la kwanza dakika ya 34 na la pili dakika ya 38, yote akisetiwa na kiungo kutoka Hispania, Alejandro Pozuelo Melero aliyemsetia pia Mjamaica Leon Bailey kufunga la tatu dakika ya 48.
Katika mchezo huo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Europa League, Samtta alifunga bao la pili la Genk dakika ya 47, baada ya Leon Bailey kutangulia kuifungia timu hiyo kwa penalti dakika ya 36.
Mabao ya wenyeji yalifungwa na Mirko Maric kwa penalti dakika ya 52 na Ivan Fiolic dakika ya 59.
Genk sasa itahitaji sare ya bila mabao au ushindi mwembamba hata wa 1-0 katika mchezo wa marudiano Alhamisi ijayo Uwanja wa Luminus Arena, Genk ili kufuzu makundi.
Genk imefika hatua hii baada ya kuitoa Cork City FC ya Ireland kwa ushindi wa jumla wa 3-1, baada ya kushinda 1-0 nyumbani na 2-1 ugenini.

No comments:

Post a Comment