Polisi mkoani Kigoma imewatia mbaroni watu watano akiwemo askari
mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa tuhuma za
kutengeneza vyeti bandia vya kitaaluma, miongoni mwake vikiwemo 90 vya uuguzi,
ambavyo vilikutwa vikisubiri kugawiwa kwa wahusika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui alisema kuwa pamoja na vyeti
hivyo vya uuguzi vilivyokamatwa, pia katika operesheni hiyo walikamata vyeti 37
vya wataalamu wa maabara na vyeti tisa vya ufamasia.
Alisema kuwa katika operesheni hiyo iliyofanywa kwa pamoja na
maofisa kutoka Baraza la Wafamasia nchini, walikamata jumla ya vyeti 936 vikiwa
kwenye hatua ya ukamilishaji vikiwa bado havijaandikwa majina, miongoni mwake
vikiwemo vyeti 667 vya wauguzi wasaidizi, vyeti 126 vya wataalam wa maabara, cheti
kimoja cha mafunzo ya afya ya jamii na vyeti viwili vya utoaji huduma ya
kwanza.
Katika kuhakikisha wanakuwa na uthibitisho wa tuhuma hizo,
Kamanda Mtui alisema kuwa pia wamekamata mihuri 25 ya taasisi mbalimbali
ikiwemo nyundo mbili, ambazo hutumika kutengenezea mihuri mbalimbali ya moto.
Aliwataja watu waliokamatwa katika operesheni hiyo ambayo
inahusisha mtandao wa watu mbalimbali kuwa ni askari wa JWTZ, Mgeni Nyamubozi
ambaye ni mume wa mmiliki wa Duka la Vifaa vya Ofisi la Upendo, lililopo Mwanga
mjini Kigoma, ambalo linatuhumiwa kuhusika na utengenezaji wa vyeti hivyo.
Katika duka hilo, Kamanda huyo wa polisi alisema polisi
walikamata kompyuta mpakato moja, ikiwa na nakala za vyeti mbalimbali za vyuo
na idara za serikali.
Mwingine aliyekamatwa ni Dickson Mshahili, muuguzi katika
Hospitali ya Mkoa Kigoma ambaye katika upekuzi nyumbani kwake, alikutwa na
nyaraka mbalimbali ikiwemo madaftari 12 yakiwa na kumbukumbu za vyeti
anavyotengeneza na mihuri ya waganga wakuu wa mikoa ya Kigoma, Kagera, Mwanza,
Singida na Tabora.
Sambamba nao alikamatwa Zawadi James, muuguzi wa Kituo cha Afya
Ujiji ambaye baada ya kupekuliwa nyumbani kwake, alikutwa na vyeti vitatu na
kabuleta ya pikipiki ambayo hutumika kutengeneza mihuri ya moto.
Wengine waliokamatwa ni Johnson Nyabuzoka, mwanafunzi wa Shule
ya Sekondari Mlole ya mjini Kigoma, ambaye ni mtaalam wa kompyuta aliyekuwa
akitumika kufanya kazi hiyo; na Stephano Erasto ambaye alikamatwa katika siku
yake ya kwanza tangu ajiunge na duka hilo kwa ajili ya kusaidia kazi.
No comments:
Post a Comment