KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa hajamuita mshmabuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Emmanuel Ulimwengu katika kikosi cha wachezaji 20 watakaosafiri mwishoni mwa mwezi huu kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017) dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles.
Ulimwengu hajacheza mwezi wote huu kutokana na kuwa na majeruhi, lakini tayari ameanza mazoezi kwa wiki mbili baada ya kupata ahueni. Mkwasa pia hajamuita Juma Abdul wa Yanga ambaye aliumia katika mchezo wa kuwania Kombe la Shirikisho dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria.
“Tanzania hatuwezi kupuumza mchezo huu, tumeuchukulia serious (kwa umakini) kabisa kwa sababu tunacheza ugenini ambako matokeo mazuri yanaweza kutusongesha mbele na kuingia ndani ya timu 99 bora katika viwango vya FIFA,” amesema Mkwasa.
“Timu itaingia kambini Agosti 28, itakaa kambini kwa siku tano kabla ya kusafiri kucheza mchezo huo wa kukamilisha ratiba ambao Misri tayari wameshafuzu fainali za Afrika,” amesema Mkwasa na kuongeza kuwa kuna mchezaji wa Tanzania, Said Carte Mhando anamfuatilia ili ikiwezekana baadaye amwite kuchezea timu ya taifa. Anakipiga Klabu ya Brencia Calcio ya Italia.
Wachezaji walioitwa; Makipa Deogratius Munishi'Dida' (Yanga) na Aishi Manula (Azam FC),Kelvin Yondani (Yanga), Vincent Andrew (Yanga), Mwinyi Hajji, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Shomari Kapombe (Azam FC) na David Mwantika (Azam FC).
Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Shiza Kichuya (Simba SC), Ibrahim Jeba (Mtibwa Sugar), Jonas Mkude (Simba SC), Muzamil Yassin (Simba SC), Juma Mahadhi (Yanga) na Farid Mussa (Teneriffe ya Hispania).
Washambuliaji ni Simon Msuva (Yanga SC), Jamal Mnyate (Simba SC), Ibrahim Hajib (Simba SC), John Bocco (Azam FC) na Mbwana Samatta - CK Genk ya Ubelgiji.
No comments:
Post a Comment