MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta atakutana na Lokomotiva Zagreb ya Croatia katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania hatua ya makundi ya Europa League.
Droo ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) iliyopangwa leo mjini Nyon, Uswisi KRC Genk ya Ubelgiji itamenyana na Lokomotiva Zagreb ya Croatia.
Mechi ya kwanza itachezwa Alhamisi Agosti 18 mjini Zagreb na marudiano yatakuwa Alhamisi ya Agosti 25 Uwanja wa Luminus Arena, Genk.
Samatta usiku wa jana alicheza vizuri Uwanja wa Turner's Cross, mjini Cork, Ireland na kuiwezesha KRC Genk kushinda 2-1 ugenini dhidi ya Cork City FC ya Ireland.
Na Genk inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-1, baada ya wiki iliyopita kushinda 1-0 mjini Genk.
Mabao ya Genk jana yalifungwa na Thomas Buffel dakika ya 12 na Sebastien Dewaest dakika ya 41, wakati la wenyeji lilifungwa na Alan Bennett dakika ya 63.
Na Samatta aliyewekewa ulinzi mkali na mabeki wa Cork City FC, alicheza kwa dakika 77 kabla ya kumpisha Bryan Heynen kumalizia mechi hiyo.
No comments:
Post a Comment