Friday, 26 August 2016

SAMATTA APIGA BAO SAFI NA KUTINGA HATUA YA MAKUNDI EUROPA LEAGUE 2016


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amefunga bao la kwanza timu yake, KRC Genk ya Ubelgiji ikishinda 2-0 na kufuzu hatua ya makundi ya Europa League usiku huu.
Katika mchezo huo wa marudiano hatua ya mwisho ya mchujo dhidi ya Lokomotiva Zagreb ya Croatia Uwanja wa Luminus Arena, Genk, Samatta alifunga bao la kwanza dakika ya pili tu akimalizia pasi ya Mjamaica, Leon Bailey.
Ni Bailey ndiye aliyeifungia Genk bao la pili dakika ya 50 katika mchezo ambao Samatta alimpisha Mgiriki Nikolaos Karelis dakika ya 80 na timu hiyo inafuzu kwa ushindi wa jumla wa 4-2 baada ya sare ya 2-2 katika mchezo wa kwanza.

Nahodha huyo wa Tanzania, Alhamisi iliyopita alifunga pia bao moja KRC Genk ikitoa sare ya 2-2 Uwanja wa Maksimir mjini Zagreb.
Samatta aliingia katika mchezo wa leo, akitoka kufunga mabao mawili Genk ikishinda 3-0 dhidi ya wenyeji, Lokeren Uwanja wa Daknamstadion mjini Lokeren Jumapili katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji.
Genk imefika hatua hii baada ya kuitoa Cork City FC ya Ireland kwa ushindi wa jumla wa 3-1, baada ya kushinda 1-0 nyumbani na 2-1 ugenini.
Kikosi cha KRC Genk kilikuwa; Bizot, Walsh, Dewaest, Colley, Uronen, Heynen, Ndidi, Pozuelo/Kumordzi dk81, Bailly/Kebano dk73 Trossard na Samatta dk79/Karelis.
Lokomotiva; Zagorac, Bartolec, Rozman, Maric, Fiolic, Peric, Grezda/Coric dk45, Sunjic, Capan/Ivanusec dk65, Bockaj/Cekici dk72 na Majstorovic.

No comments:

Post a Comment