Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano hapa Nchini (TCRA) imewaonya
watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaojisajili katika mitandao hiyo kwa kutumia
majina na taarifa za uongo.
James Kilaba Kaimu Mkurugenzi wa TCRA amesema, vitendo vya watu
kujisajili katika mitandao ya kijamii kwa kutumia majina na taarifa zisizo
sahihi, ni kosa kisheria na kwamba wanaofanya hivyo watachukuliwa hatua kali za
kisheria.
Kilaba ameyasema hayo jana, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya
kuongeza ufahamu kuhusu matumizi sahihi na salama ya mitandao ambayo
inasimamiwa na Kitengo cha dharura cha kuitikia matukio ya usalama kwenye
mitandao hapa nchini (TZ-CERT).
“Tumeamua kuzindua
kampeni hii ili kuwasaidia wananchi kuepuka makosa ya kimtandao na kuepuka
kufanyiwa utapeli au wizi mitandaoni kwa sababu matukio mengi ambayo yamekuwa
yakiripotiwa au kulalamikiwa yanazuilika kwa watu kupewa elimu ya matumizi
sahihi ya mitandao,” alisema Kilaba.
Kampeni hiyo ya kuongeza ufahamu kuhusu matumizi sahihi na
salama ya mitandao, itafanyika kupitia matangazo ya redio, televisheni,
magazeti pamoja na mitandao ya kijamii ambapo katika mitandao ya kijamii
itajulikana kama, “Darasa mtandao”.
“Miongoni mwa mambo
ambayo tutawafundisha wananchi ni kutoweka wazi taarifa zao binafsi zote katika
mitandao, kubadili na kutunza neon la siri (password), kutojibu ujumbe unaosema
umeshinda bahati nasibu na mengineyo mengi,” alisisitiza Kilaba.
No comments:
Post a Comment