Tuesday, 16 August 2016

REFA BORA KUCHEZESHA YANGA NA AZAM KESHO TAIFA


REFA bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, Ngole Mwangole wa Mbeya atachezesha mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam FC.
Katika mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni, Mwangole atasaidiwa na Josephat Bulali na 
Frank Komba wa Dar es Salaam.

Refa wa akiba atakuwa Soud Lila wa Dar es Salaam pia, wakati Kamisaa Peter Temu wa Arusha.

Kiingilio cha chini katika mchezo huo kinatarajiwa kuwa Sh. 5,000 kwa majukwaa ya mzunguko, wakati VIP B na C itakuwa Sh. 15,000 na VIP A 20,000.

Pazia la msimu mpya linafunguliwa leo kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga SC na Azam FC, ambao utakuwa mchezo wa nne kwa timu hizo kukutana mwaka huu pekee.

Awali timu hizo zilikutana katika mechi tatu za mashindano matatu tofauti, Yanga ikishinda moja na kutoka sare mara mbili.

Januari 5, timu hizo zilitoa sare ya 1-1 kwenye Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, Machi 5, zikatoa sare ya 2-2 kabla ya Yanga SC kushinda 3-1 Mei 25, katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka laTanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Katika mchezo wa huo, Azam FC itakuja na benchi jipya la Ufundi chini ya makocha kutoka Hispania watupu chini ya Zeben Hernandez Rodriguez, wakati Yanga itaendelea kuongozwa na Mholanzi Hans van der Pluium anayesaidiwa na mzalendo, Juma Mwambusi. 
 
Na kwa ujumla, kwenye Ngao ya Jamii hii itakuwa mara ya nne mfululizo Yanga na Azam kukutana tangu mwaka 2013. Na katika mechi zote za awali ni Yanga SC waliobuka kifua mbele dhidi ya Azam. Mwaka 2013 Yanga walishinda 1-0 bao pekee la Salum Telela, aliyeachwa msimu huu na kuhamia Ndanda FC ya Mtwara, 2014 walishinda 3-0 Mbrazil Genilson Santana ‘Jaja’ akifunga mabao mawili na mwaka jana walishinda kwa penalti 8-7 baada ya sare ya 0-0.

Yanga wataingia kwenye mchezo wa kesho wakitokea hoteli ya Tiffany katikati ya Jiji, walipoweka kambi yao, wakati Azam FC watatokea kwenye hosteli zao za Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment