Waziri wa Habari,
Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye (kulia) akitoa tamko la
kufungia vituo viwili vya redio ambavyo ni Kituo cha Redio Five Arusha na
Magic FM Dar es Salaam kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo
jijini Dar es Salaam, kutokana na kukiuka Kanuni za Sheria ya
Utangazaji ya mwaka 2005 kwa kurusha hewani vipindi vyenye maudhui ya
uchozezi,na Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Uratibu wa Vyombo vya Habari Bw.
Jamal Zuberi wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo.
Baadhi ya waandishi wa
Habari wakifuatilia tamko alilokuwa akitoa Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na
Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye (hayupo pichani) la kufungiwa kwa
Redio Five Arusha na Redio Magic FM Dar es Salaam leo
Agosti 29,2016 Jijini Dar es Salaam.
Tamko la kufungwa kwa
vituo hivyo vya redio limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri
wa Habari, Utamaduni ,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari.
Aidha,Waziri Nape
alivitaja vituo hivyo kuwa ni Kituo cha Redio Five cha Arusha na Kituo cha
Redio Magic FM Dar es Salaam na alisisitiza kuwa utekelezaji wa
tamko hilo unaanza leo tarehe Agosti 29, 2016 mara baada ya kutangazwa.
“Uamuzi wa kuvifungia
vituo hivyo umefikia baada ya kujiridhisha kuwa kipindi cha MATUKIO
kilichorushwa tarehe 25 Agosti ,2016 muda wa 02:00 usiku hadi 03:00 usiku na
Kituo cha Utangazaji cha Redio Five Arusha na kipindi cha
cha Morning Magic katika kipengele cha KUPAKA RANGI kilichorushwa
tarehe 17 Agosti, 2016 kati ya saa 01:00 asubuhi na saa 02:00 asubuhi vilikuwa
na maudhui ya uchochezi unaoweza kuleta uvunjifu wa amani na hivyo kukiuka
masharti ya kanuni ya 5 (a),(b),(c) na (d) pamoja na Kanuni ya Huduma za
Utangazaji (Maudhui) za mwaka 2005”, alisema Waziri Nnauye.
Waziri huyo mwenye
dhamana na vyombo vya habari nchini alisema vituo hivyo vimefungiwa kwa muda
usiojulikana na ameelekeza Kamati ya Maudhui kuviita vyombo hivyo na kuwasikiliza
kwa kina zaidi na kumshauri hatua zaidi za kuchukua kwa mujibu wa Kanuni za
Utangazaji za mwaka 2005.
Pamoja na hayo Waziri
Nape alivitahadharisha vyombo mbalimbali vya habari
,kutoshawishika kuvunja Sheria na Kanuni zinazoongoza tasnia ya
Habari ili kulinda heshima ya tasnia ya habari na kuhakikisha nchi
inabaki na Amani.
Hata hivyo Sheria
ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ya mwaka 2003 Kifungu cha 28 (1)
kimempa Mamlaka Waziri wa mwenye dhamana na masuala ya Habari kufungia vyombo
vya habari vinavyoweza kurusha hewani habari za uchochezi.
No comments:
Post a Comment