Friday 26 August 2016

WATU 3 WAKUTWA WAMEFARIKI HUKU BAADHI YA SEHEMU ZA MIILI YAO KULIWA NA WANYAMA MKOANI GEITA

Watu 3 wamegunduliwa wakiwa wamefariki  huku  baadhi ya sehemu za miili yao kuliwa na wanyama katika eneo la mlima Kitongo  wilaya ya Nyangwhale mkoani Geita.

Tukio hilo limegunduliwa august 22 majira ya saa saba mchana katika kijiji hicho kilichopo katika kata ya Kakora wilaya ya Nyangwhale mkoani hapa ambapo marehemu hao waliotambulika kwa Leticia Charles 40, Salu Nyanda 65 na Frola Thomas 2 wote wakiwa ni wakazi wa kijiji hicho wamekutwa wamefariki umbali wa mita 200 kutoka barabara kuu ya kijiji hicho.

Inadaiwa kuwa kati ya julai 22 na 27 mwaka huu majira ya saa mbili usiku marehemu waliondoka nyumbani wakidaiwa kuelekea kwa mganga wa kienyeji aitwaye Ndutu Maswila 65 mkazi wa kijiji cha Nyangalamila kwa ajili ya kupata tiba  na tangu hapo hawakuonekana tena hadi walipogunduliwa wakiwa wamefariki na baadhi ya miili yao kuliwa na wanyama.

Aidha katika eneo la tukio zimekutwa nguo zilizotambuliwa kuwa ni za marehemu hao , sufuria mbili zikiwa kwenye mafiga huku ndani kukiwemo dawa za miti shamba huku pembeni kukiwa na mafuvu mawili.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Mponjoli Mwabulambo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema jeshi la polisi linaendelea na upelelezi ili kubaini kiini cha tukio na baadae kuwakamata wahusika wa tukio hilo.

No comments:

Post a Comment