Rais Mstaafu wa Awamu ya
pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Ally Hassan Mwinyi ametoa wito kwa
watanzania kuongeza juhudi katika kupiga vita dhidi ya ujangili nchini.
Wito huo umetolewa leo
jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu cha “Tembo-Faru wana haki ya
kuishi Tanzania” kilichoandaliwa na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa
Dar es salaam.
Rais mstaafu huyo,
amesema kumekuwa na tatizo la kutowalinda na kuwatunza wanyama hao kwani
kuwauwa ni dhambi na kinyume na kusudio la Mungu kwa kuwa wanyama hao wana haki
ya kuishi kama viumbe wengine.
“ kumekuwa na matukio
mengi ya uuaji wa wanyama wakiwemo tembo na faru na hivyo kupunguza rasilimali
ya taifa kwa vizazi vijavyo na pia kitendo hicho ni kinyume na kusudio la Mungu
hivyo ni vizuri kuwatunza, kuwapenda, kuwaendeleza na kuwalinda wanyama hao
kwani ni moja ya vivutio vinavyochangia pato la Taifa” aliongeza Rais Mstaafu Mwinyi.
Kwa upande wake Waziri
wa Maliasili na Utalii Prof Jumanne Maghembe amesema kuwa Tanzania ni nchi ya
pili kwa kuwa na mbuga nzuri duniani hivyo ni budi kushirikiana katika
kupambana dhidi ya ujangili ndani ya nchi yetu.
Ameongeza kuwa jumuiya
ya ujangili ni kubwa ambayo inahusisha mifumo mbalimbali ikiwemo
watengenezaji wa silaha za kuua tembo, waagizaji wa meno ya tembo, wasambazaji
na watu mashuhuri ambao wanatumia nyumba zao kuhifadhi meno ya tembo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya WILDAID Peter Knights ambao ni wadhamini
wa kitabu hicho, ameipongeza Serikali ya China kwa jitihada zake za kupiga
marufuku biashara ya uuzaji wa meno ya Tembo hatua hiyo imesaidia kulinda
wanyama hao.
Kitabu cha Tembo-Faru
wana haki ya kuishi Tanzania kimetayarishwa na kamati ya Amani ya Viongozi wa
Dini Mkoa wa Dar es salaam kikiwa na lengo la kudumisha amani kwa binadamu na
Wanyama ili wasiweze kupoteza uhai wao.
No comments:
Post a Comment