Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeamua kulifungia kwa miezi 36 gazeti la “MSETO”.
Amri ya kulifungia Gazeti hilo imetolewa kwa Tangazo la Serikali Na. 242
lililotolewa tarehe 10 Agosti, 2016. Uamuzi huo umetolewa kwa mujibu wa Sheria
ya Magazeti ya Mwaka 1976 Sura ya 229, kifungu 25(1).
Kifungu hicho
kinasema “Waziri akiona kwamba
kwa ajili ya manufaa ya umma au kwa ajili ya kudumisha amani na usalama inafaa
afanye hivyo aweza kutoa amri na kuitangaza kwenye Gazeti la Serikali ambayo
itaeleza kwamba gazeti lililotajwa katika amri hiyo litakoma kutolewa tangu
siku (ambayo katika fungu hili itaitwa ''tarehe ya kuanza kutumika'')
itakayotajwa katika amri hiyo”
Uamuzi huo unazuia
gazeti la Mseto kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na
mitandao (Online publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki
na Posta Sura ya 306.
Aidha, hatua hii ya
kulifungia gazeti hilo imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi
kubwa za muda mrefu kuanzia Septemba, 2012 hadi Agosti, 2016
kumtaka Mhariri wa gazeti kuacha kuandika habari za upotoshaji, uchochezi na za
uongo na zisizo zingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari bila
mafanikio.
Kutokana na hali hiyo,
Serikali kwa masikitiko makubwa, imelazimika kuchukua uamuzi huu kutokana na
mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo wa kuandika na kuchapisha habari ya uongo
na kughushi kwa kutumia nyaraka mbalimbali za Serikali kwa nia ya kumchafua Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wa
Serikali kwa lengo kutaka kumchonganisha na wananchi ambao wamekuwa na
matarajio makubwa kwa uongozi wa Awamu ya Tano.
Pamoja na makosa
mengine, hivi karibuni gazeti lao katika toleo Na. 480 la tarehe 4 hadi 10
Agosti, 2016 lilichapisha na kusambaza makala na barua ya kugushi kutoka
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) yenye kichwa cha habari kisemacho
“Waziri Amchafua JPM” Amhusisha na rushwa ya uchaguzi mkuu, ni Naibu Waziri wa
Ujenzi, Mawasiliano.
Kwa mujibu wa vyombo
vya uchunguzi vya Serikali, imebainika kwamba nyaraka hiyo imeghushiwa na
wahariri na walipotakiwa kuleta uthibitisho wa nyaraka waliyotumia katika gazeti
lao, walishindwa kuleta vithibitisho hivyo
Ninatoa wito kwa
wamiliki, wahariri, waandishi na watangazaji wa habari kuzingatia sheria,
kanuni na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ambayo ukizingatiwa
hakutakuwa na migogoro yoyote. Aidha Serikali inasisitiza kwamba inaheshimu
uhuru wa vyombo vya habari unaozingatia maadili, weledi na Sheria za nchi na
kwamba Serikali itaendelea kushirikiana navyo.
Serikali ya Tanzania
imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayoanisha uhuru na mipaka ya habari
kama vile Tamko la Kimataifa la haki za Binadamu la mwaka 1948, Mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, na Mkataba wa Afrika juu ya Haki za
Binadamu na Watu 1981.
Mikataba na matamko
hayo kwa pamoja licha ya kuanisha uhuru wa habari ambao Tanzania imeruhusu kwa
kiwango kikubwa pia, imeweka ukomo wa uhuru huo kwa kukataza habari za uongo,
uzushi na uchochezi.
No comments:
Post a Comment