Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametoa siku 14 kwa maofisa wanaohusika na udhibiti wa dawa za kulevya kwenye mpaka wa Tunduma mkoa wa Songwe, kuwakamata watu wanaohusika na uvushaji wa dawa hizo kutoka nchini kwenda nchi jirani ya Zambia na nyingine zilizopo ukanda huo.
Nchemba alitoa agizo hilo jana, alipofanya ziara ya kukagua mpaka huo, ambapo alisema ni jambo lisilofichika kuwa kwa sasa Tanzania imechafuka kutokana na dawa za kulevya.
Alisema kutokana na
Watanzania wengi kukamatwa katika nchi mbalimbali duniani, wakijihusisha na
usafirishaji wa dawa za kulevya, imefikia hatua kwa baadhi ya nchi kufikiria
kuongeza masharti zaidi kwa kila atakayejitambulisha kuwa Mtanzania.
“Hatuwezi kuacha nchi ikachafuka kwa sababu tu
ya watu wachache.Ukienda China Watanzania zaidi ya 200 wanashikiliwa kwa dawa
za kulevya, Pakistan wapo, India, Afrika Kusini ni Watanzania. Hili
linatuchafua sana,” alisema Nchemba.
Aliutaja mpaka wa
Tunduma kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa kupitisha dawa hizo na kutaka
nguvu kuongezwa zaidi ili kuwezesha misako.
Alisema wapo watu
ambao si makondakta wa mabasi wala abiria, lakini wamekuwa wakisafiri kila siku
kwenye mabasi, hatua inayodhihirisha kuwa ndiyo wanaojihusisha na usafirishaji
wa bidhaa hizo haramu.
Alisema watu hao
wamekuwa na ushirikiano na watu wengine katika miji ya jirani, kabla ya kufika
mpakani ikiwemo kijiji cha Mpemba wilayani Momba mkoani Songwe, ambapo wakifika
hapo basi husimamishwa na mzigo kushushwa, kisha kusafirishwa kwa njia za panya
hadi ng’ambo ya nchi.
“Wakati ninyi mnafanya utaratibu wa kawaida wa
kupitisha gari husika hapa mpakani, wao wanavusha kupitia njia za panya. Basi
likishavuka na mzigo unakuwa umefika Zambia wanakutana na kuupakia tena kisha
wanaendelea na safari.
“Na katika hili ni lazima mzungumze pia na wenzenu wa upande wa pili, wadhibiti pia mji unaofuata baada ya huo wa mpakani maana huko ndiko wanakopakia tena. Kama mtashindwa katika wiki mbili, nitakuja mimi mwenyewe na nitawakamata tu,” alisisitiza.
“Na katika hili ni lazima mzungumze pia na wenzenu wa upande wa pili, wadhibiti pia mji unaofuata baada ya huo wa mpakani maana huko ndiko wanakopakia tena. Kama mtashindwa katika wiki mbili, nitakuja mimi mwenyewe na nitawakamata tu,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment