Tuesday, 2 August 2016

MO DEWJI AANZA FUJO SIMBA, AMWAGA MILIONI 100 ZA USAJILI

MFANYABIASHARA Mohamed Gulam Dewji ametoa mfano wa hundi Sh. Milioni 100 kama mchango wake katika usajili wa klabu hiyo kuelekea msimu ujao.

Mo Dewji ametoa mfano wa hundi hiyo leo ofisini kwake, jengo la Golden Jubilee, Tower, Mtaa wa Ohio, Dar es Salaam akimkabidhi Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva.

Na Aveva akamshukuru Mo Dewji kwa msaada huo, lakini akasema bado wanahitaji Sh. Milioni 320 kukamilisha usajili, ingawa hakusema bajeti nzima ya usajili ya klabu hiyo ni kiasi gani.

“Ninashukuru sana kwa msadaa huu kutoka kwa mwanachama wetu, na sasa ninashukuru tunaweza kumsajili Frederick Blagnon kutoka Ivory Coast,”alisema Aveva. 

Mo Dewji aliahidi kuchangia usajili wa Simba iwapo wanachama wa klabu hiyo watakubali mabadiliko kutoka kwenye mfumo wa klabu kumilikiwa na wanachama wote hadi kuuza hisa.

Na Mkutano wa Jumapili Bwalo la Maofisa wa Polisi, Dar es Salaam ulikubali kuingia kwenye mchakato wa kuuza hisa.

Na Mo alitoa sharti hilo sambamba na ofa ya kununua asilimia 51 ya hisa za klabu kwa Sh. Bilioni 20 iwapo mabadiliko yatapitishwa. 

Na wakati akipokea mfano wa hundi hiyo leo, Aveva alisema ameyakubali mabadiliko kwa moyo mmoja na atayasimamia kuhakikisha yanakwenda haraka ili kutimiza azma ya Simba kuwa ya kutisha siyo tu Tanzania, bali Afrika nzima.

Pamoja na hayo, Aveva akawataka wanachama zaidi wa Simba kuchangia sehemu iliyobaki, Sh. Milioni 320 katika bajeti ya usajili ya klabu.

“Usajili unaendelea haujafika ukingoni, zoezi ambalo lina gharama kubwa, natoa wito kwa wanachama wengine wa Simba, waige mfano huu. Isije ikatokea ikasemwa kwamba Simba imefunga usajili kwa sababu Mo katoa fedha, hapana. Ametoa kiasi kidogo na mwingine akijitokeza hata kumfuata ofisini kwake kama hivi atukabidhi, tupo tayari,”alisema Aveva. 

No comments:

Post a Comment