Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) imetoa ufafanuzi juu ya utozwaji wa kodi za misaada inayotolewa
na wadhamini kusaidia Sekta ya Maendeleo ya Michezo Nchini.
Ufafanuzi huo
umetolewa leo na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo
kutokana na habari iliyochapishwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuhusu
Serikali kukosa mabilioni ya fedha kwa sababu ya kutokukusanya kodi ya fedha
zinazotolewa na wadhamini kwenda kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF).
“Fedha zinazotolewa
kama msaada kutoka kwa wadhamini huwa hazikatwi kodi lakini TRA hupata mapato
yake kutokana na matumizi ya fedha hizo hasa pale wahusika wanapozitumia katika
shughuli za kiuchumi”,alisema Kayombo.
Kayombo ametaja baadhi
ya shughuli za kiuchumi zinazoweza kuwaingizia mapato kutoka kwenye misaada
hiyo kuwa ni; kodi za waajiriwa wakiwemo makocha na wachezaji, makusanyo ya
uwanjani ,kupewa huduma za kitaalam pamoja na majengo ya kupangisha au kupanga.
Amefafanua kuwa kama
Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) linakodisha jengo basi
fedha wanazopata lazima walipe kodi ya asilimia 10 kutoka kwenye fedha hizo na
kama wao ndio wamekodi jengo kwa ajili ya matumizi yao wanatakiwa kutoa kodi ya
asilimia 5.
Kwa upande wa kodi
kutoka kwa waajiriwa, Mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kwa vilabu vya
michezo kuwa michezo ni ajira kama ajira zingine hivyo mishahara yao inatakiwa
kukatwa kodi kulingana na kiasi wanacholipwa.
Zoezi la kuwatoza kodi
makocha na wachezaji limeanza rasmi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment