Naibu Mwanasheria mkuu wa Serikali Mhe. Gerson
Mdemu akiongea na wajumbe kutoka Serikalini na Asasi za Kiraia wakati wa
ufungaji wa kikao kuhusu mapendekezo yaliyotolewa kwa serikali wakati wa
majadiliano ya taarifa ya nchi ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu
chini ya mfumo wa mapitio kwa kipindi maalum na baraza la haki za binadamu la
umoja wa mataifa, Leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Masuala ya
Katiba na Haki za Binadamu Kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi.
Sarah Mwaipopo.
Wajumbe kutoka Serikalini na Asasi za Kiraia
wakimsikiliza Naibu Mwanasheria mkuu wa Serikali Mhe. Gerson Mdemu wakati wa
ufungaji wa kikao kikao kuhusu mapendekezo yaliyotolewa kwa serikali wakati wa
majadiliano ya taarifa ya nchi ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu
chini ya mfumo wa mapitio kwa kipindi maalum na baraza la haki za binadamu la
umoja wa mataifa, Leo Jijini Dar es Salaam.
Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeendelea kushikilia msimamo wake wa kupinga ndoa
za jinsia moja,kuongeza uwigo wa uhalalishaji wa utoaji mimba,adhabu
ya kifo,kuweka sera ya kutonyonga wanaokutwa na adhabu ya kifo na uridhiwaji wa
mikataba ya Kimataifa inayozuia masuala ya utesaji kwa kuwa masuala hayo
yanaonekana kutoendana na Katiba na Sheria za nchi, Sera,mila desturi na tamaduni
za watanzania ikiwa ni sehemu ya mapendekezo 72
yaliyokataliwa na Serikali wakati wa mapitio ya taarifa ya nchi ya
ukuzaji na usimamizi wa haki za binadamu.
Naibu Mwanasheria Mkuu
wa Serikali Ndugu Gerson Mdemu ameyasema hayoleo jijini Dar es Salaam alipokuwa
akifunga kikao maalumu cha siku mbili cha wadau mbalimbali wa
masuala ya haki za binadamu ambapo ameeleza kuwa Serikali ilipokea
jumla ya mapendekezo 227 yaliyotolewa na Baraza la Haki za
Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Mei 2016 chini ya mfumo wa mapitio kwa
kipindi maalum (The Universal Periodic Review).
Mdemu ameongeza kuwa mapendekezo
hayo kwa ujumla yalijikita katika majukumu ya Tanzania kwenye mikataba
ya kimataifa ,Mifumo ya kikatiba na kisheria,miundombinu ya kitaasisi ya haki
za binadamu ,masula ya kisera,ushirikiano na vyombo vya kikanda na
kimataifa,utawala wa sheria,uendeshaji haki,masuala ya kulinda haki za msingi
za binadamu kama vile haki ya kuishi,haki ya afya,haki za walemavu,watoto,haki
ya habari na kujieleza,afya elimu mazingira haki za watu asilia na wakimbizi.
Hata hivyo, Tanzania
ilikubali kutekeleza mapendekezo 130 tu kati ya 227 yaliyokuwa yanahusu
mchakato wa Katiba,kuijengea uwezo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,
kuhuisha Sera za nchi ili ziendane na malengo endelevu ya Dunia ,kuandaa
taarifa za nchi za utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu na kuziwasilisha
kwenye vyombo vya vya umoja wa mataifa kwa wakati.
Vilevile Serikali
iliahirisha jumla ya mapendekezo 25 ambayo yalijikita katika marekebisho
ya sheria ya Takwimu, 2015, Sheria ya makosa ya mtandao, 2015,ukamilishaji wa
Sheria ya Habari, Sheria ya vyombo vya Habari,uandaaji wa mikakati na
mipangokazi ya utekelezaji wa msuala ya kuzuia ndoa za utotoni na za
kulazimishwa ,upitishaji wa sera mpya mbalimbali ikiwemo ya kutoa vyeti vya
kuzaliwa na usajili wake kuwa bure na masuala ya uchaguzi Zanzibar, kwa
lengo la kuyapitia tena kwa kina na kushirikisha zaidi wadau ili hatimaye
kuweka msimamo stahiki kabla mapendekezo hayo hayajawasilishwa tena Baraza la
Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa hatua za mwisho za kupitisha rasmi
taarifa ya nchi katika kukuza na kulinda haki za Binadamu.
Aidha, Naibu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametumia fursa hiyo kusisitiza kuwa
Serikali itaendelea kulinda na kukuza haki za bindamu ikiwa ni pamoja na
kupokea hoja na maoni ya wadau ili kuboresha taarifa ya nchi itakayowasilishwa
katika Baraza la Haki za Binadamu la umoja wa mataifa kabla au ifikapo tarehe 9
Septemba, 2016 na kuwataka watanzania wote kushiriki ipasavyo katika dhana
nzima ya kukuza na kulinda haki za bindamu nchini.
Utaratibu wa Mapitio
kwa kipindi maalum (The Universal Periodic Review) wa masuala ya haki za
binadamu ulianzishwa na Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2006 kwa lengo la
kuzifanyia mapitio nchi 192 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa, Tanzania
ikiwa miongoni, kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa masuala ya kulinda na
kukuza haki za binadamu nchini mwao.
No comments:
Post a Comment