Fisi |
Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya
Magharibi kinamsaka fisi mmoja kati ya wawili waliowashambulia Samwel Gamalaya
na kusababisha kifo chake na kumjeruhi Kusekwa Ngeleja wakati wakikata kuni
katika pori lililopo Kitongoji cha Isukamahela Manispaa ya Tabora.
Fisi hao wawili walimshambulia kwa kumng’ata
Gamalaya maeneo mbalimbali ya mwili na kusababisha kifo chake, huku wakimjeruhi
Ngeleja mikono na miguu.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya
Magharibi, Charles Msilanga alisema jana (juzi) kuwa baada ya polisi kumpiga
risasi fisi mmoja na kumuua, mwingine alikimbia.
Alisema wanaendelea kumsaka fisi huyo ili kuzuia
madhara zaidi kwa wakazi wa kitongoji hicho.
“Fisi aliyekimbia anaweza kuleta madhara kwa watu
na ndiyo maana tunamsaka kwa udi na uvumba,” alisema Msilanga.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Iddi Cheyo alisema
Gamalaya alifariki dunia baada ya kukaa muda mrefu bila matibabu tangu
aliposhambuliwa na fisi hao.
Baadhi ya wakazi wa kitongoji hicho, Sophia
William na Juma Kapambala walisema tukio hilo limewastaajabisha kwani kwa miaka
mingi wanafanya shughuli zao ndani ya msitu huo bila kushambuliwa na wanyama.
“Tunafanya shughuli zetu katika msitu huu kwa
miaka mingi bila kuvamiwa, lakini hatujaona mnyama kuingia eneo hilo,” alisema Sophia.
No comments:
Post a Comment