Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi NEC,Jaji mstaafu Damian Lubuva.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu
Damian Lubuva, amesema mchakato wa Kura ya Maoni ya Katiba mpya umeanza baada
ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Kauli hiyo ya Jaji Lubuva imekuja wakati wadau wa siasa nchini
wakimtaka Rais Dk. John Magufuli, kutoendelea na Kura ya maoni badala yake
mchakato wa Katiba mpya urudi nyuma na baadhi ya mambo yaliyo kwenye Katiba
iliyopendekezwa yarekebishwe.
Ikumbukwe kuwa mchakato wa Katiba mpya uliingia dosari baada ya
baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupinga mfumo wa Serikali Tatu
uliokuwa umependekezwa na Tume ya Jaji mstaafu Joseph Warioba, iliyokusanya
maoni nchi nzima na matokeo yake kuzaa kundi lililojiita Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA).
“Tulikuwa tunangoja tumalize uchaguzi, unamaliza mmoja unakwenda
kwa mwingine. Sasa tumemaliza (uchaguzi mkuu), tunakwenda kwa lingine (Kura ya
Maoni),”alisema Jaji Lubuva.
Alienda mbele zaidi na kusema “Tunaliangalia,kama Tume
tutakuja kuwajulisha wananchi hali ikoje, tuliahirisha Kura ya Maoni ili
tumalize hili (uchaguzi mkuu).”alisema Jaji Lubuva.
Alipoulizwa kuhusu makadirio ya bajeti ya kuendesha kura hiyo ya
maoni, Lubuva alisema: “Hilo niulize siku nyingine, sina zaidi ya hapo
kwa leo.”
Rais Magufuli alipokuwa akihutubia Bunge la 11 siku ya
kulizindua Novemba 20, mwaka jana, alisema serikali yake imepokea kiporo cha
mchakato wa Katiba ambao haukukamilika katika awamu iliyomtangulia kutokana na
kutokukamilika kwa wakati wa uandikishaji wapiga kura.
“Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa
ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji
wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba
lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu kama
ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba,” alisema Rais Magufuli.
Mbali na muundo wa serikali tatu, baadhi ya mambo ambayo Ukawa
walitaka yawe kwenye Katiba mpya ni mamlaka ya Rais kupunguzwa, ushindi wa Rais
uwe zaidi ya asilimia 50, Tume huru ya Uchaguzi, matokeo ya Rais kupingwa
mahakamani, kuwe na mgombea binafsi, mawaziri wasitokane na wabunge, na muundo
mpya wa Bunge la Muungano
No comments:
Post a Comment