Mwanasheria mkuu wa serikali, George Masaju amesema mahakama
maalumu ya mafisadi inasukwa na itatekelezwa kwa muundo wa mahakama, ikiwa ni
kitengo ndani ya Mahakama Kuu.
Masaju alisema Muswada wa Sheria ya kuanzisha Mahakama
Maalumu ya Mafisadi uko tayari na utawasilishwa Aprili mwaka huu bungeni, kwa
ajili ya kujadiliwa na kupitishwa kuwa sheria, kutoa nafasi kwa mahakama hiyo
kuanza kazi.
“Mahakama ya mafisadi na wala rushwa ipo, tunaisuka na
itatekelezwa kwa muundo wa mahakama zetu, itakuwa ni kitengo maalumu ndani ya
Mahakama Kuu, kinachoshughulika na masuala ya ufisadi na rushwa,” alisema Masaju.
Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita, usiku, kwenye
kipindi cha Siku 100 za Serikali ya Awamu ya Tano kinachorushwa na Kituo cha
Utangazaji cha Taifa cha TBC1, Mwanasheria huyo alisema mchakato wa uanzishwaji
wake uko kwenye hatua nzuri kabla ya kuwasilishwa kwenye mkutano wa Bunge ujao.
Alisema ana imani wabunge wote wataunga mkono muswada huo
kwa kuwa ni suala la Watanzania.
Akizungumza kwenye mkutano wa pili wa Bunge la 11, Waziri wa
Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema wizara yake imeanza maandalizi
ya muswada huo wa kuanzisha Mahakama Maalumu ya mafisadi.
Dk Mwakyembe alisema wanafanyia kazi suala hilo kwani ahadi
iliyotolewa na Rais lazima ifanyiwe kazi na ufumbuzi uwepo. Aidha Mwakyembe
alisema wananchi wavute subira kwa sababu mambo mazuri hayahitaji haraka na
mchakato wake ukikamilika watajulishwa.
Rais John Magufuli alipohutubia wakati wa ufunguzi wa Bunge,
Novemba 20,mwaka jana, aliendelea kusisitiza mapambano dhidi ya rushwa na
ufisadi akisisitiza juu ya azma ya kuanzisha mahakama hiyo.
Alisema vitendo vya rushwa na ufisadi vyenye madhara makubwa
kwa nchi na ustawi wa nchi, hutendwa na watu wenye dhamana kubwa za uongozi na
utumishi, ambazo wamezipata kutokana na ridhaa ya watu.
Katika kushughulikia tatizo hilo, aliahidi kuunda Mahakama
ya Rushwa na Ufisadi na kusema ana matumaini vyombo husika havitamkwamisha.
No comments:
Post a Comment