Makontena bandarini |
WADAIWA 16 waliokwepa kulipa kodi ya Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), baada ya kutorosha kontena za mizigo yao kwenye Bandari Kavu
(ICD) ya Azam mwishoni mwa mwaka jana, mali zao zinaanza kukamatwa leo na
kufilisiwa.
Mkurugenzi wa Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono,
iliyopewa kazi ya kufuatilia wadaiwa hao wakiwemo baadhi ambao wamekamilisha
malipo, Yono Kevella alisema hayo Dar es Salaam jana.
Akizungumza, Kevela alisema kuanzia leo wanakaa na vyombo
vya dola, kuanza utaratibu wa kukamata na kufilisi mali za wahusika na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Kevela alisema hadi sasa hakuna zuio lililotolewa,
linazowazuia kutekeleza wajibu wao katika kukusanya madeni hayo. Hata hivyo
alisema, wengi wa wadaiwa baada ya kutolewa kwa muda huo wa siku 14, wameonesha
moyo wa kulipa.
Wadaiwa 16 hawajamaliza madeni Alitaja wadaiwa 16 ambao
hawajalipa madeni yao wala kupunguza, ambao watafilisiwa wasipojitokeza kufanya
malipo ni Said Ahmed Said Sh 28,249,352.50, Strauss International
(45,393,769.95), Farid Abdallah Salum (52,185, 614.97).
Wengine ni Nasir Saleh Mazrui (60,105,873.77), Simbo Yona
Kimaro (64,221,009.10), Ally Masoud Dama (102,586,719.22) na Juma Kassem Abdul
(130,182,395.12), Salum Link Tyres (233,447,913.31) na Tybat Trading Co.Ltd
(448,690,271.90).
Pia wamo IPS Roofing Co.Ltd (966,723,692.10), Tuff Tyres
General Co Ltd, (7,435,254,537.03), Swalehe Mohamed Swalehe (34,687,165.00),
Rushwheel Tyre General Co Ltd, (1,802,988,679.20), Said Ahmad Hamdan
(68,362,558.31), Ahmed Saleh Tawred ( 59,237,578.40) na Farida Abdullah Salem
Sh 75,334,871. 85.
Akizungumzia wadaiwa waliolipa ndani ya siku 14 walizopewa
na zikaisha juzi, alisema wanane kati ya 24, ndiyo walijitokeza kulipa madeni
baada ya kampuni yake kuwafuatilia.
Kevela alisema hadi jana zaidi ya Sh milioni 200 zimelipwa
na wadaiwa hao.
Wadaiwa hao 24 walishindwa kulipa kodi kwa wakati kama
walivyotakiwa kufanya, ndipo TRA ilimpa dalali huyo kazi ya kuwafilisi. Kampuni
hiyo ya udalali ilitoa siku 14, kuanzia Februari 10, mwaka huu wawe
wamekamilisha; muda ambao umeisha juzi.
Kevela alisema katika siku hizo 14, kati waliojitokeza
kulipa,wanne kati yao wamemaliza madeni na wengine wanne wamepunguza madeni na
kuahidi kumalizia kiasi kilichobaki. Waliomaliza madeni yao Wadaiwa waliolipa
madeni yao yote ni Issa Ali Salim aliyekuwa akidaiwa Sh 94,543,161.96, Libas
Fashion (26,593,245.78), Omary Hussein Badawy (21,346,615.40) na Zulea Abas Ali
(16,760577.24).
Waliopunguza madeni yao Waliopunguza madeni yao ni Zuleha
Abbas Alli aliyelipa Sh milioni 47 na kubakiwa na deni la Sh 28,508,551, awali
alikuwa akidaiwa Sh 75,508,551.88, mwingine ni Ally Awes Hamdani aliyelipa Sh
milioni 17.26 awali alikuwa akidaiwa Sh 55,485,904.07).
Wengine waliopunguza kidogo ni Tifo Global Trading Co Ltd
waliolipa Sh milioni mbili ilhali deni lao ni Sh 1,573,300,644.58, Lotai Steel
Tanzania Ltd, waliolipa Sh milioni mbili ilhali deni lao ni Sh
5,476,475,738.19.
“Tulikabidhiwa wadaiwa 24 na TRA, waliokwepa kodi kwa
kutorosha kontena katika bandari kavu ya Azam mwishoni mwa mwaka jana, sasa
walipewa muda wa kulipa ila walikaidi, tukakabidhiwa tuwafilisi mali zao zote
ili kulipia madeni na wamejitokeza hao na kuanza kulipa wengine wamemaliza”, alisema Kevela.
Awali wadaiwa 24, walikwepa kodi ya Sh bilioni 18.95 kwa
kutorosha makontena 329 ya bidhaa zao kutoka Kampuni ya SSB ambayo ndiyo
mmiliki wa bandari kavu ya (Azam ICD) na kampuni ya Regional Cargo Services.
Mapema Desemba mwaka jana aliyekuwa Kaimu Kamishna wa TRA,
Dk Philip Mpango alizungumza na waandishi wa habari na kusema kampuni 15 kati
ya 43, zilizokwepa kodi baada ya kutorosha kontena 329 katika ICD ya Azam,
wamelipa.
Dk Mpango alisema Desemba 12, mwaka jana ndiyo ilikuwa siku
ya mwisho aliyotoa Rais John Magufuli ya siku saba kwa wakwepa kodi hao 43,
kulipa wenyewe kwa hiari, vinginevyo sheria zitachukua mkondo wake. Kufuatia
kauli hiyo ya Rais Magufuli, wadaiwa 15 walijitokeza na kulipa na waliobaki
hawakujitokeza kulipa.
No comments:
Post a Comment