Friday 26 February 2016

WAZIRI MKUU APOKEA MCHANGO WA VIFAA VYA BILIONI 10 VYA MAHOSPITALI KUTOKA AZAM,COKE NA PEPSI.


              Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitazama baadhi ya vitu vilivyotolewa.



     Mkurugenzi wa IPP Reginard Mengi akislimiana na Waziri mkuu Mh.Kassim Majaliwa.

Umoja wa Wazalishaji Vinywaji laini umetoa msaada wa vifaatiba vyenye thamani ya Sh10 bilioni vilivyopokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Vifaatiba vilivyopokelewa jana ni pamoja na mashine za aina mbalimbali kama utra sound, mashine za kustulia moyo, vitanda vya watoto njiti, vitanda vya kujifungulia, vitanda 80 vya kawaida na magodoro yake, ambavyo viliwekwa kwenye makontena 20.

“Haijapata kutokea msaada mkubwa kama huu,” alisema Majaliwa kwenye hafla hiyo iliyofanyika kwenye ghala la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) iliyoko Mabibo, Ubungo jijini Dar es Salaam. 
 “Natoa wito kwa makampuni mengine binafsi kuunga mkono jitihada za Serikali.”

Msaada huo wa vifaa tiba unawalenga zaidi watoto na wajawazito, ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kuboresha huduma za afya.

Msemaji wa umoja huo, Erastus Mtui kutoka Coca Cola Kwanza alisema msaada huo umelenga kusaidia watoto na wajawazito pamoja na wagonjwa wengine kama wa moyo.

“Tumelenga hasa vifaa vya watoto na wajawazito. Hii yote ni katika kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli kwani anaboresha afya na kutokomeza rushwa, hii inayaokoa zaidi makampuni ya uzalishaji nchini,” alisema Mtui.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Majaliwa alizipongeza sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali kukabiliana na changamoto katika sekta ya afya.

Alisema vifaa hivyo vimekuja wakati mwafaka kwa kuwa vitawezesha vituo kutoa huduma bora za afya.
Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Rais Magufuli alihamasisha maboresho ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hasa wodi ya wazazi, hatua hii mliyoichukua ya kutoa msaada wa vifaa hivi ni sehemu ya kumuunga mkono,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema Serikali kupitia MSD itahakikisha vifaa hivyo vinasam bazwa kwenye vituo husika kwa umakini mkubwa, hasa maeneo yenye mahitaji makubwa.

Alisema tayari kuna orodha ya awali katika mikoa ya Dodoma, Geita, Katavi, Lindi, Kilimanjaro, Mara, Mbeya, Shinyanga na Tanga.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema bohari imedhamiria kusambaza dawa na vifaa tiba vya kutosha kwenye kanda nane za nchi, lakini changamoto kubwa ni jinsi ya kuzihifadhi.

Ukubwa wa ghala hili la vifaa tiba ni mita za mraba 19,650 na hapa panatugharimu kiasi cha Sh2.5 bilioni. Na iwapo tutaendelea kuhifadhi hapa, itatulazimu kulipia Sh4 bilioni,” alisema Bwanakunu na kuongeza kuwa:

Kwa hiyo changamoto ni kupata eneo la kujenga ghala. Wizara ya Ardhi ikitupatia eneo, tunategemea kuanza ujenzi mara moja.” 

Wafanyakazi PSI wasimamisha ziara
 Wafanyakazi wa kampuni ya PSI walisimamisha msafara wa Waziri Mkuu kwa kuziba barabara wakati akiondoka, wakitaka wamuambie kero wanazokumbana nazo kazini.

Wafanyakazi hao walitoa kero zao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulipwa malipo kiduchu kiasi cha Sh5,750 kwa siku, huku wakinyimwa kushiriki kuchangia mfuko wa hifadhi ya jamii wa PPF.

Shida yetu kubwa ni mshahara. Tangu mwaka 2013 tunalipwa Sh5,750 mpaka leo na kwa miaka yote hiyo watu hawashiriki PPF,” alisema Amini Athuman ambaye ni mfanyakazi wa PSI.
Wote ni vibarua, hakuna aliyeajiriwa hapa. Pia kinamama wajawazito hawalipwi chochote wakienda kujifungua, mtu anafukuzwa kazi bila kosa lolote bosi akiamua.”

Akijibu malalamiko hayo, Waziri Mkuu alisema ameyapokea na kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ilishajipa kazi ya kusikiliza kero za wananchi na wafanyakazi, lazima tatizo hilo litatuliwe.

Nawasihi kesho (leo) mje kazini asubuhi saa 2:00 asubuhi na Waziri ya Kazi, Jenister Mhagama atakuwa hapa kwa kuwa mmelalamika kwamba hata makato ya PPF hayakatwi. Namsihi kiongozi ayaandike vizuri malalamiko ili akija asome kwa umakini na utatuzi utapatikana kesho hiyohiyo. Nawasihi msigome kufanya kazi,” alisema. 

No comments:

Post a Comment