Wachimbaji
wadogo wa mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Tamko lililotolewa na Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassan kuwa wachimbaji wadogo watapewa mabaki ya mawe ya dhahabu maarufu
magwangala kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) limesababisha wakazi wa Mtaa
wa Nyakabale kufurika mgodini hapo kusubiri ahadi hiyo.
Vijana hao zaidi ya 800 walisema kuwa
wamekusanyika kwa kuwa Serikali ilitangaza kutoa magwangala Februari 28.
Akizungumza na umati wa vijana hao Kaimu Ofisa
Madini wa Mkoa wa Geita, Fabian Mshai aliwataka vijana hao kuwa watulivu na
kutii sheria za nchi kipindi hiki ambacho tume iliyoundwa kufuatilia suala la
magwangala, imepeleka maoni kwa katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
kujua utaratibu utakaotumika.
Mshai alisema lazima taratibu zifuatwe ili
kuepuka kuhatarisha uhai wa wananchi kwa kugombana wakati wakinyang’anyana
mawe.
Alisema pia wanaweza kuharibu mazingira kwa kuwa
kuna kemikali kali zinazotumika wakati wa uchanjuaji wa dhahabu.
Alisema kitendo kinachofanywa na wachimbaji
wadogo walioamua kuanza kuingia katika maeneo ya mgodi na kuchukua mawe ni
kukiuka sheria za madini na kuhatarisha maisha yao.
Diwani wa Mgusu, Pastory Ruhusa aliwataka
wachimbaji wadogo kuwa watulivu na kuiomba Serikali kuharakisha taratibu za
kutoa magwangala kwa kuwa kuna ongezeko kubwa la wananchi kutokana na ahadi
waliyopewa.
Alisema, juzi vijana hao walifunga barabara baada
ya kuitwa wakimbizi na kusababisha wananchi kushindwa kusafiri kwenda nje ya
kijiji na kusababisha usumbufu kwa wagonjwa na wananchi. 0.3k 0 0 0 0 0
No comments:
Post a Comment