Makamu wa raisi Mh.Samia Suluhu Hassan.
Makamu wa raisi akipokelewa mara baada ya kuwasili Tanga.
Wakati sakata la kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam likiendelea kupamba moto
baada ya mchakato huo kuwekewa zuio la mahakama juzi, serikali imetishia
kuivunja Halmashauri ya Jiji la Tanga iwapo haitamaliza mgogoro wake wa
kisiasa.
Akizungumza na
viongozi serikali na kisiasa jijini Tanga jana, Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan, alisema serikali italazimika kuivunja halmashauri hiyo endapo mgogoro
huo hautamalizwa haraka, kutokana na ukweli kwamba tangu kuanza kwa uongozi wa
awamu ya tano baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana imeshindwa kufanya vikao
vyake halali kwa mujibu wa katiba kutokana na mgogoro wa kisisa bina ya Chama
Chama cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa, huku wananchi
wakishindwa kutatuliwa kero zao kwa wakati hivyo kuzorotesha maendeleo yao.
“Mpaka sasa jiji la Tanga hakuna uongozi uliosimama, sasa hatuwezi
kwenda kwa mwendo huu, wananchi wanahitaji maendeleo na kurudia uchaguzi
hatuwezi ni gharama kubwa, kilichobaki ni kuivunja halmashauri mpaka hapo muda
wa kufanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya nchi utakapotimia, hivyo kwa maana
nyingine kama itavunjwa serikali kuu ndiyo itasimamia shughuli za jiji hili,” alisema Suluhu.
Alisema mkoa huo una
mipango mbalimbali ya maendeleo lakini haiwezi kutekelezeka kutokana na mgogoro
uliopo na kuwataka viongozi wa mkoa kwa kushirikiana na wazee kukaa chini
kutafuta namna ya kuumaliza haraka.
“Jiji ni kioo cha mkoa
mzima, sasa kama wazee hawatakaa kitako na viongozi kutafuta suluhu, basi hii
mipango yenu yote ya kufufua viwanda itakuwa ni ndoto tu kwa sababu hapa mjini
hakupo shwari na tunalitambua hilo,” alisema.
Mgogoro wa umeya Tanga
umeibuka baada ya CCM yenye madiwani wachache kushinda nafasi hiyo dhidi ya
Ukawa yenye madiwani wengi jambo ambalo linapingwa na umoja huo unaondwa na
vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.
Hatua kama hiyo ya
kuvunja halmashauri si mara ya kwanza kutokea nchini, kwani mwaka 1996,
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilivunjwa na serikali na badala yake
ikaundwa Tume ya Jiji iliyokuwa chini ya Charles Keenja.
Makamu wa Rais pia
alisema mkoa wa Tanga unakabiliwa na changamoto kubwa ya biashara ya magendo,
hali ambayo inarudisha nyuma mkoa huo kiuchumi na kimaendeleo.
Kufuatia hatua hiyo
aliiagiza kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kutumia kila mbinu kuzuia
biashara hiyo ili mkoa uweze kuimarika kiuchumi na kimapato.
Kuhusiana na suala la
chakula, Makamu wa Rais alisema serikali ya awamu ya tano haitamvumilia mkuu wa
mmoa yeyote wala wilaya ambaye atatoa malalamiko ya kukosekana kwa chakula
kwenye eneo lake na badala yake atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.
Alisema kukosekana kwa
chakula wakati viongozi wa eneo husika wana uwezo wa kujenga malambo ili
kukinga maji ya mvua kipindi cha masika na kuwaelekeza wananchi kulima mazao
yanayostahimili ukame, itakuwa ni kipimo chao cha uongozi na wale ambao
watashindwa kupata madawati kwa ajili ya shule kwenye maeneo yao.
Awali akisoma taarifa
ya mkoa wa Tanga kwa Makamu wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza,
alisema hali ya chakula mkoani humo hadi kufikia mwezi huu si ya kuridhisha
kutokana na kuchelewa kunyesha kwa mvua msimu wa mwaka 2014/2015 na hata
ziliponyesha hazikuwa na mtawanyiko mzuri.
No comments:
Post a Comment