Sunday 28 February 2016

USHINDI MKUBWA KWA CLINTON SOUTH CAROLINA KATIKA UCHAGUZI WA MCHUJO WA URAISI.

Hillary Clinton ameshinda kwa wingi wa kura uchaguzi wa mchujo wa urais katika jimbo la South Carolina dhidi ya mpinzani wake mkuu katika chama chao cha Democratic Bernie Sander.
Bi Clinton alipata kura asilimia 84, miongoni mwa wapiga kura wengi ambao ni watu wenye asili ya Kiafrika katika jimbo hilo.
Aliahidi katika hotuba yake ya ushindi kuwa ataendelea kupigania kila kura katika majimbo yote yaliyosalia na kuwa hatapuuza lo lote.
Huku akigusia kura za mchujo za Jumanne Kuu au ijulikanavyo kama ''Super Tuesday'', Bi Clinton alisema kuwa kura hizo za uchaguzi sasa zimechukua mkondo wa kitaifa.
Bernie Sanders alimpongeza Bi Clinton kwa ushindi wake lakini akasema mambo bado.
Bi Clinton alimshinda Sanders kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa, hii ikiashiria kuwa Clinton alipata kura 8 kati ya 10 zilizopigwa na wapigaji kura wamarekani weusi.
Ushindi huo ni wa tatu kwa bi Clinton katika kinyang'anyiro hichi cha kumtafuta mshika bendera wa chama cha Democratic.
Clinton alikuwa ameshinda majimbo ya Iowa na Nevada.
Mpinzani wake mkuu bwana Sanders ndiye aliyeshinda jimbo la New Hampshire.
Miaka 8 iliyopita bi Clinton alishindwa huko South Carolina kwa rais Barack Obama.
''Nafkiri kuwa kauli yenu imetuma tahadhari kubwa kote nchini kuwa sote tunasimamia na kukubaliana kuwa pamoja twaweza.''alisema bi Clinton.
Bi Clinton vilevile alimtupia jiwe mgombea anayepigiwa upatu katika chama cha Republican bwenyenye Donald Trump.

''Kwa hakika hatustahili kuzungumza eti tunaitaka Marekani kuwa bora tena ...haifai ,,,Marekani haijawahi kudorora ! Marekani ni nchi bora zaidi na yenye nguvu zaidi duniani.'' aliongezea bi Clinton.

No comments:

Post a Comment