Naibu Spika Dk. Tulia Mwansasu, amepata ajali mkoani Mbeya
alikokwenda kwa ajili ya mapumziko. Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Rungwe,
Zainab Mbussi, Dk. Tulia alipata ajali hiyo jana wakati akitokea Mbeya mjini
akielekea Kyela.
Mkuu wa wilaya alisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Shule
ya Sekondari ya Kipoke iliyoko wilayani humo.
Alisema maelezo ya askari wa usalama barabarani, yanaeleza kuwa
chanzo cha ajali hiyo ni gari dogo lililoelezwa kuwa liliibeba familia ya mtu aliyetajwa
kwa jina moja la Chacha, lililokuwa likitokea Kyela kwenda Mbeya, lilipojaribu
kulipita lori na kukutana na gari la Naibu Spika.
Mbussi alisema Dk. Tulia, mdogo wake pamoja na mlinzi wake
waliokuwa kwenye gari lake wako salama ingawa gari hilo limeharibika vibaya
sehemu za mbele.
Aidha, alisema baadhi ya abiria waliokuwa kwenye gari la Chacha
wakiwemo wanawe wawili walipata majeraha na walipelekwa katika hospitali ya
Mission Igogo, Kiwira.
Awali mapema jana, Dk. Tulia, alitoa msaada wa sh. milioni tano,
ili kulifanyia ukarabati bweni la Mapinduzi, ambalo alikuwa analala
wakati anasoma Shule ya Sekondari ya Wasichana Loleza, iliyopo jijini Mbeya.
Dk. Tulia ambaye alisoma shuleni hapo kuanzia kidato cha
kwanza hadi cha nne, mwaka 1991 hadi 1994, pia alitoa msaada wa magunia mawili
ya mchele kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi.
Akizungumza na walimu na wanafunzi, Dk.Tulia alisema ametajiwa
changamoto nyingi, zinazoikabili shule hiyo na kuwa amzichukua na kuahidi
kutafuta wadau atakaoshirikiana nao ili waweze kusaidia kuzitatua.
Dk. Tulia alisema ameguswa na uchakavu wa mabweni, ambapo
alipata fursa ya kuonyeshwa yakiwemo mawili aliyokuwa analala akiwa shuleni
hapo, ambayo ni Kibo linaloendelea kutumika hadi sasa na lile la Mapinduzi
ambalo kwa sasa halitumiki.
“Kwenye bweni nililokuwa
nikikaa nimepita mwenyewe. Naahidi kushughulika na lile bweni la Mapinduzi
ndilo lililo kwenye hali mbaya zaidi kiasi cha kushindwa kuendelea kutumika,” alisema Dk.Tulia.
Dk.Tulia alitoa magunia mawili ya mchele, kwa ajili ya chakula
kwa wanafunzi shuleni hapo na aliwachekesha wanafunzi pale aliposema katika
mambo ambayo hayajabadirika shuleni hapo ni ratiba ya kula wali mara mbili kwa
wiki.
“Kwa sababu mimi dada
yao nimewatembelea leo, na waswahili wanao msemo ‘mgeni njoo mwenyeji apone’,
basi mimi nitawaletea magunia mawili ya mchele ili angalau kwa hizi wiki
wanafunzi wawe wananikumbuka,” alisema
Dk.Tulia.
Naye, mbunge wa Songwe, Philip Mulugo, alimuunga mkono Dk.Tulia
kwa kuchangia sh. milioni moja, kwa ajili ya kusaidia ukarabati wa bweni hilo
la Mapinduzi.
Viongozi mbalimbali wa Chama na serikali, wakiongozwa na Mkuu wa
Wilaya ya Mbeya, Munasa Nyerembe, walikuwepo katika ziara hiyo na Naibu Spika
kutembelea shule hiyo ambayo hivi sasa inachukua wanafunzi wa kidato cha tano
na sita tu.
No comments:
Post a Comment