Dkt.Joyce Ndalichako, Waziri wa elimu,sayansi,teknolojia na mafunzo ya ufundi.
Anguko la shule za sekondari za Serikali zikiwamo za vipaji
maalumu katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, limedaiwa kusababishwa na
walimu kukata tamaa, miundombinu duni na mazingira magumu ya kufundishia na
kusomea.
Shule za vipaji maalumu, zinazochukua wanafunzi wanaofanya
vizuri katika mtihani wa darasa la saba, hazimo kwenye orodha ya shule 50 bora,
na kati yao ya kwanza inashika nafasi ya 53.
Orodha hiyo imetawaliwa na shule binafsi na za taasisi zisizo za
serikali, hasa za kidini wakati za Serikali zinapambana kuanzia nafasi ya 53.
Kukata tamaa kwa walimu na mazingira magumu ya kufundishia ndiko
kumeelezwa na wachambuzi mbalimbali kuwa ndiyo sababu kuu ya kuporomoka kwa
kiwango cha ufaulu kwa shule hizo.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alitaja shule 10
bora juzi kuwa ni Kaizirege ya Kagera, Alliance Girls (Mwanza), St Francis
Girls (Mbeya), Alliance Boys (Mwanza), Canossa (Dar es Salaam), na Marian Boys
(Pwani).
Nyingine ni Alliance Rock Army (Mwanza), Fedha Girls (Dar es
Salaam), Feza Boys (Dar es Salaam) na Uru Seminary (Kilimanjaro).
Huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa Kaizirege kuongoza katika
mitihani ya kitaifa huku Alliance Boy na Girls zikiwamo pia katika 10 bora kwa
miaka mitatu mfululizo.
Anguko la shule za Serikali
Kuanguka kwa shule hizo kumedhihirika juzi mara baada ya
kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha nne ambayo sehemu kubwa hazikufanya
vizuri.
Dk Msonde alizitaja baadhi ya shule za sekondari za vipaji
maalumu kuwa ni Ilboru ambayo imeshika nafasi ya 53, Kibaha (69), Kilakala
(94), Mzumbe (71), Tabora Boys (124), Tabora Girls (128) na Msalato (148).
Akizungumzia hatua hiyo, Meneja wa Utafiti na Sera wa Taasisi ya
Hakielimu, Godfrey Boniventure alisema anguko hilo linaonyesha wazi kuwapo kwa
tabaka kubwa kati ya walionacho na wasio nacho.
“Shule zote 10 za mwisho ni za Serikali ambazo wanasoma watoto
wa maskini. Kibaya zaidi hata za vipaji maalumu zilizokuwa zikitegemewa zipo
hoi. Hii ni hatari kwa Taifa,” alisema.
Alisema tabaka hilo litawafanya watoto wanaotoka kwenye familia
zenye uwezo kupata nafasi za juu kwenye soko la ajira, huku maskini wakishindwa
kuingia kwenye ushindani huo.
Profesa wa Chuo Kikuu Ruaha (RUCU), Gaudence Mpangala alisema
anguko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kukata tamaa kwa walimu.
Alisema walimu hawana moyo wa kuendelea kufanya kazi hiyo na
utafiti kwenye baadhi ya shule unaonyesha wengi wao wanaingia darasani
kukamilisha ratiba na si kufundisha.
Profesa Mpangala alisema sababu iliyowafanya kufikia hatua hiyo
ni Serikali kutowalipa stahiki zao kama mishahara, motisha, makato na mazingira
magumu ya kufundishia.
“Ilitokea kwangu.
Niliamua kumhamisha mwanangu aliyekuwa akisoma shule ya vipaji maalumu kwa
sababu walikuwa hawaingii darasani, sikuwalaumu hata kidogo, niliona wazi
mazingira yao ya kazi ni magumu.”
Alisema sera ya elimu bure itachangia anguko kubwa zaidi
kutokana na hali ya shule hizo kuendelea kuwa mbaya. “Majengo ya shule za vipaji maalumu
yamechoka, Serikali haipeleki pesa na wazazi hawachangii. Kitakachotokea hapo
ni kufeli zaidi,” alisema.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitila Mkumbo
alisema kukata tamaa kwa walimu kunachangia shule hizo kufanya vibaya.
Aliitaka Serikali kurejesha hadhi ya shule zake ili ziendelee
kuwa kimbilio la wanyonge.
“Kiwango cha walimu katika ufundishaji kimeshuka kwa kiwango kikubwa, Serikali
isipotoa kipaumbele kwa kundi hili, itakuwa hatari zaidi,” alisema.
Ilboru wanena
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ilboru, Julius Shura
alikiri kuwa hali ya shule hiyo ni taabani kutokana na kuchakaa kwa
miundombinu.
“Hata hivyo, tumejitahidi
kutoa wanafunzi wawili bora ambao wametokana na jitihada zetu walimu licha ya
kuwa mazingira ya kufundishia ni magumu. Tunaomba Serikali itupie jicho shule
hizi ambazo zilikuwa taa kwa watoto wa Kitanzania wenye vipaji maalumu,”alisema.
“Hali ni ngumu zaidi kwa
watoto wenye ulemavu, hakuna mazingira rafiki hata kidogo. Piga picha bajeti ya
Sh1,500 kwa mtoto anayesoma sayansi ni ndogo sana kwa siku, usitegemee kwamba
atafanya maajabu,” alisema.
Siri ya shule binafsi kuongoza
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na
Vyuo Visivyo Vya Serikali (Tamangsco), Benjamin Nkonya alisema siri ya shule
zao kuongoza ni kuwekeza kwa walimu.
“Tunawasikiliza
walimu, kuwapa heshima wanayostahili na kuhakikisha wanapatiwa kila
wanachohitaji kama mikopo ya magari na nyumba, ukimjali mwalimu mengine yote
yatakwenda vizuri,” aliongeza .
No comments:
Post a Comment