Thursday 18 February 2016

AMANI NA UTULIVU KUIMARISHWA ZANZIBAR.


Waziri wa mambo ya ndani mheshimiwa Charles Kitwanga.

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema imejipanga kuhakikisha inaimarisha amani na utulivu kwenye marudio ya uchaguzi Mkuu wa Zanzibar mwezi ujao na kukamilisha uchaguzi huo kwa ufanisi.

Kutokana na hilo, Waziri Charles Kitwanga amesema atakwenda katika visiwa vya Unguja na Pemba vinavyounda Zanzibar ili kufuatilia tuhuma za baadhi ya askari Polisi kutumika kuwazuia baadhi ya watu kupiga kura katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Machi 20, mwaka huu.

Akifungua kikao cha maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi jana Dar es Salaam, Kitwanga alisema ameridhishwa na polisi walivyojipanga kuhakikisha uchaguzi huo wa Zanzibar unafanyika kwa amani.

Alisema anaungana na jeshi hilo kuhakikisha Pemba na Unguja wanafanya uchaguzi huo kwa amani na kudhibiti wote watakaojaribu kuleta vurugu huku akimtaka Kamishna wa Zanzibar kusimamia suala hilo.

Katika kuongeza nguvu, mimi mwenyewe hivi karibuni nitatembelea huko Pemba ili kuhakikisha askari hao wanadhibitiwa,” alisema Kitwanga.

Waziri ikiwa ni mara yake ya kwanza kukutana na viongozi wote wa Jeshi la Polisi wa nchi nzima tangu ateuliwe Desemba mwaka jana, alitoa pongezi kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu.

Mlisimamia kwa weledi wa hali ya juu Uchaguzi Mkuu katika muda wote wa mchakato, mlisimama imara kabla, wakati na baada ya uchaguzi na kudumisha amani, utulivu, umoja na mshikamano kwa Watanzania wote,” alisema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Awali, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu alisema kwa sasa wanaendelea kujipanga kuimarisha amani na utulivu kwenye marudio ya uchaguzi huo wa Machi 20 na kuahidi kukamilisha jukumu hilo kwa ufanisi.

Alitumia fursa hiyo kuomba ushirikiano wa wananchi na wadau wote wa uchaguzi ili kuweka mazingira mazuri na salama kwa wananchi kutumia haki yao ya kuchagua viongozi kama ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana aliosema ulikuwa na ushindani mkali kuliko ilivyowahi kutokea siku za nyuma, lakini hali ya amani na utulivu ilidumishwa.


No comments:

Post a Comment