Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Paul Makonda.
Moja ya jambo ambalo
serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa John Pombe
Magufuli imelifanya kuwa kipaumbele kikubwa kwenye mipango yake ya kimaendeleo
ni suala la uboreshaji wa sekta ya elimu nchini na ndio maana serikali imeanza
utekelezaji wa mpango huu kwa kufuta ada zote mashuleni.
Kimsingi ni ndoto hii ya Mheshimiwa Raisi ambayo nina hakika
kila mmoja wetu anaelewa ukubwa wa faida zake kwenye ujenzi wa Tanzania mpya na
yenye wasomi na wataalamu wa kila namna tena wanaopatikana bila kuzingatia hali
ya kipato cha familia anayotokea mwanafunzi, iliyonifanya mimi kama msaidizi
wake katika nafasi ya ukuu wa wilaya nijiulize kila wakati juu ya ushiriki
wangu wa kuhakikisha inatimia kikamilifu.
Maswali ambayo yamenifikisha kwenye wazo la kuboresha sekta hii
kwa kuchagua kufanya jambo ambalo wakati serikali ikiendelea kupigania
changamoto nyinginezo za kuboresha ajira za walimu ikiwemo upandishwaji wa
madaraja na mishahara, basi na mimi katika nafasi yangu nishiriki kwenye
mchakato huu mzima kwa kutoa motisha ya usafiri wa bure kwa walimu wote
wanaofundisha kwenye shule za serikali zilizopo jijini Dar es Salaam.
Kwa ufupi ni kwamba, wazo hili limejengwa juu ya msingi wa
sababu kubwa tatu. Moja, kwa kuzingatia changamoto za nauli za mara kwa mara
wanazolazimika kuzilipa walimu ili kuyafikia kwa wakati maeneo yao ya kufanyia
kazi na pili, ni kuhakikisha mimi na serikali yangu ya wilaya ya Kinondoni
tunakuwa sehemu ya juhudi za Mheshimiwa Raisi za kuboresha maslahi na mazingira
ya walimu ya kufanyia kazi ili matarajio ya ndoto yake anayoipigania usiku na
mchana ya kutaka kuiona sekta ya elimu nchini ikikua kwa kasi yanatimia.
Na tatu, ni kuwafanya walimu wa wilaya ya Kinondoni na Dar es
Salaam kwa ujumla kama watumishi wenzangu wa serikali nao wanafaidi sehemu ya
matunda ya serikali yao ambayo kwa dhati imedhamiria kubadilisha maisha yao ili
na wao waweze kubadilisha maisha ya vijana wetu kupitia taaluma.
Kwasababu hizo nilizozianisha hapo juu ninaomba kuwatangazia
walimu wangu wa shule zote za serikali kuanzia za msingi mpaka sekondari ya
kwamba, sasa watasafiri bure wanapokwenda kutufundishia wadogo zetu na watoto
wao.
Hii ni baada ya kufanya vikao na mazungumzo ya kina na wamiliki
wa vyombo vya usafiri wa umma kupitia vyama vyao vya Darcoboa na Uwadar na
hatimaye mazungumzo hayo kuitimishwa na mkutano wa vyama vyote hivyo viwili vya
wamiliki wa vyombo vya usafiri ambao kwa sauti moja wamekubali kuniunga mkono
kwenye utekelezaji wa wazo langu hili.
Kipekee na kwa unyenyekevu mkubwa, naomba kuchukua fursa hii
kuwashukuru sana wamiliki hawa wa vyombo vya usafiri wa umma pamoja na viongozi
wa vyama vya Darcoboa na Uwadar kwani walikuwa na kila sababu ya kukataa hasa
ukizingatia kuwa wao ni wafanyabiashara na tena wanazo changamoto nyingi katika
sekta yao ya usafirishaji, wengine wakiwa hata wamekopa kwenye mabenki ili
wapate uwezo wa kufanya biashara, lakini kwenye jambo hili wote kwa umoja wao
wameseme ndio na wako tayari kuanza haraka iwezekanavyo.
Utaratibu kwa walimu juu ya utumiaji wa fursa ambayo tumeipata
utakuwa kama ifuatavyo:- Moja, nimemuelekeza ofisa elimu wa sekondari na shule
za msingi, kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule zote za serikali zilizopo
wilayani kwangu na wilaya nyinginezo za jiji la Dar es Salaam, kutengeneza
vitambulisho vya shule zao vitakavyokuwa na picha ya mwalimu, jina lake kamili,
jina la shule anayofundisha, namba ya simu ya mkuu wa shule husika pamoja na
saini yangu mimi mwenyewe Paul Makonda ili kuepuka udanganyifu.
Nimewataka zoezi hili walifanye na kulikamilisha ndani ya wiki
moja ambapo baada tu ya kukamilika itakuwa ni furaha yangu kuwatangazia walimu
wote wa shule za serikali jijini Dar es Salaam kuwa, watakuwa wakipanda
daladala bure ila tu kwa siku za jumatatu mpaka Ijumaa na kwa muda wa saa kumi
na moja asubuhi mpaka saa mbili asubuhi na kati ya saa tisa mpaka saa kumi na
mbili jioni. Ingawa, kila mwalimu atalazimika kuonyesha kitambulisho chake
alichotengenezewa kwenye shule yake pamoja na kile cha ajira ya serikali.
Imetolewa na:-
Paul Makonda
Mkuu wa wilaya – Kinondoni.
No comments:
Post a Comment